Monday, November 30, 2009

WATANZANIA WASHUSHWA KWENYE NDEGE YA PRECISION AIR.

Zaidi ya abiria 15 raia wa Tanzania waliokuwa wakisafiri kwa ndege ya shirika la Precision Air kutoka Arusha kuelekea Dar es salaam, walishushwa na kupakiwa abiria wengine raia wa kigeni (wazungu) tukio hili lilitokea jana katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kusababisha mtafaruku uliodumu kwa zaidi ya dakika 30 kabla ya walinzi wa uwanja huo kuingilia kati ili kutuliza hali hiyo kutokana na abiria hao kugoma kushuka.

Wakizungumza uwanjani hapo abiria hao wamedai kuwa kitendo cha kuteremshwa katika ndege waliyopanda na kupakizwa abiria wengine ambao ni raia wa kigeni (wazungu) bila kuelezwa sababu za msingi ni kitendo cha ubaguzi wa hali ya juu sana.

Mmoja wa abiria Pamela Msuya aliyekumbwa na kadhia hiyo alisema; dakika chache kabla ya ndege kupaa hewani, rubani alizima injini ya ndege hiyo na wahudumu kuwaeleza kuwa kumetokea dharura, hivyo hawawezi kupaa. Alisema kutokana na hali hiyo, waliombwa kusubiri hadi saa 5:40 asubuhi, awali walikuwa waondoke na ndege hiyo saa 1:00 asubuhi, abiria huyo alieleza kuwa, ilipofika saa 5:40 waliingia katika ndege na rubani kuiwasha, lakini ilizimwa tena na kuamrishwa kuteremka kwa maelezo ndege hiyo ilipaswa kupakia abiria wa Zanzibar ambao ni raia wa kigeni (wazungu).
Pamela aliendelea kudai kuwa, wakiwa wanashushwa katika ndege hiyo, baadhi ya abiria waligoma na kusababisha kutokea kwa mtafaruku mkubwa wa zaidi ya dakika 30 kabla ya walinzi wa uwanja huo kuitwa na wahudumu wa ndege hiyo na kwenda kuwashusa huku wakiwaita wazamiaji. Si siri kabisa '' tumedhalilishwa sana katika ndani ya nchi yetu kabisa'' yaani tunaitwa wazamiaji mbele ya wageni, watatuelewaje? Tuna booking ya muda mrefu tofauti na hao (raia wa kigeni) alisema Pamela.

Baada ya kushushwa abiria hao, wengine ambao wengi ni raia wa kigeni walionekana wakipanda ndege hiyo kuelekea Zanzibar.

Abiria mwingine ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema alishangazwa sana na kitendo hicho kutokana na abiria hao (wazungu) kutokuwa na taarifa za usafiri (booking) na kwamba walifika muda huohuo na kupatiwa usafiri. Aliongea kuwa, baadaye walituambia tusubiri ndege ya saa tano, tukavumilia na muda huo ulipofika, tena wakatuambia tusubiri ya saa 11 jioni, huu si uungwana hata kidogo '' alisema abiria huyo''.
Baada ya jitihada za kupata uongozi wa shirika hilo kugonga mwamba, mmoja wa wafanyakazi wa Precision Air mkoani Arusha ambaye alikataa kutaja jina wala cheo chake, alisema kwa kifupi tatizo hilo linashughulikiwa.

-Ni aibu sana kwa jambo kama hili, pia ni aibu kwa nchi yetu kwa matukio kama haya, kwanini lakini?

No comments:

WATEMBELEAJI