Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (ccm) juzi jioni alimwacha hoi Waziri Mkuu Mizengo Pinda, pale alipowapa salamu ya shikamoo watoto, ili pamoja na wazazi wao wamchague tena kuwa mbunge wa Jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao.
Tukio hilo lilitokea wakati Waziri Mkuu alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Sikonge katika mfululizo wa ziara yake ya kuutembelea Mkoa wa Tabora.
Kabla ya Waziri Mkuu kuanza kutoa hotuba yake, Nkumba alipewa nafasi ya kuwasalimia wapiga kura wake, ndipo alipotumia nafasi hiyo kutangaza nia yake ya kugombea tena Ubunge.
Mbunge huyo alisema;
Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakati ulipokuwa ukiahirisha kikao cha Bunge kilichopita ulisema; sasa ni wakati muafaka kwetu sote wabunge kurudi kwa wapiga kura wetu ili kuwapa shikamoo.
Leo ni siku ya bahati kwangu kwani watu wengi wamejitokeza katika mkutano wako huu, na mimi naomba kutumia nafasi hii kutoa shikamoo. ''Kwa heshima na taadhima Shikamoo watoto wote mliopo hapa kuanzia mnaonyonya, watoto wa halaiki, watoto mliopo shuleni, na Shikamoo vijana na wazee wote mliopo hapa'' alisema Mbunge Nkumba.
Tukio hilo lilimfanya Waziri Mkuu aliyekuwa amekaa jukwaani na viongozi wengine wa Taifa, Mkoa na Wilaya, kuvunjika mbavu kwa kicheko.
Waziri Mkuu Pinda amehitimisha ziara yake jana, ya siku saba Mkoani Tabora kwa kutembelea Wilaya zote sita za; Igunga, Nzega, Tabora, Uyui, Urambo na Sikonge.
No comments:
Post a Comment