YALIYOJIRI WAKATI WA IBADAYA KUWEKWA WAKFU KWA MABALOZI WA VATICAN BARANI AFRICA, AKIWEMO RUGAMBWA KUTOKA TANZANIA. MONSIGNOR NUNZIO NOVATUS RUGAMBWA.
Rugambwa akiitwa kuwekwa wakfu.
Akiwekwa wakfu kuwa Askofu.
Rugambwa akiitwa kuwekwa wakfu.
Akiwekwa wakfu kuwa Askofu.
Somo la pili la kiswahili likisomwa na Sista Gesela Upendo Msuya.
Maaskofu Wakuu wapya. Machozi ya furaha yalionekana kumiminika kwenye shavu la mama Rugambwa, (mama mzazi wa Monsignor Novatus) wakati maandamano ya Maaskofu wakuu wateule walipokuwa wakiingia taratibu kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, siku ya alhamisi jioni, tarehe 18 Marchi, 2010.
Kulikuwa na idadi kubwa ya Makardinali, Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waamini walei, waliotoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya kushuhudia tukio hili la kihistoria katika maisha na utume wa Maaskofu wakuu wateule: Novatus Rugambwa, Piero Pioppo na Eugene Martin Nugent.
Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwa heshima ya Mtakatifu Yosef mchumba wake Bikira Maria, iliongozwa na Kardinali Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican, akisaidiwa na Askofu Nestori Timanywa wa Jimbo Katoliki la Bukoba - Tanzania, Jimbo anamotoka Askofu Mkuu Novatus Rugambwa.
Kabla ya kuwekwa wakfu, waraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa ajili ya uteuzi wao kuwa Maaskofu wakuu ulisomwa. Baba Mtakatifu amewakaribisha Maaskofu wakuu wapya kwa moyo mkujufu katika urika wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki na anawaombea mapaji ya Roho Mtakatifu ili waweze kutekeleza wajibu wao kikamilifu.
Baba Mtakatifu amewapatia zawadi ya pete ya Kiaskofu, Maaskofu wote watatu, ambao watamwakilisha Barani Afrika, mahali ambapo Baba Mtakatifu anaendeleza kuonyesha jicho na upendeleo wa kibaba. Ibada ya kuwekwa wakfu iliendelea mintarafu maelekezo ya kanuni na sheria za Kanisa Katoliki.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, somo la pili lilisomwa kwa lugha ya kiswahili na Mheshimiwa Sista Gisela Upendo Msuya. Kwa wazungumzaji wa lugha ya kiswahili, kwanza kabisa walionekana kana kwamba wamepigwa na butwaa, kwa kusikiliza matendo makuu ya Mungu yakisimuliwa kwa lugha isiyogusa akili, mioyo na utashi wao.
Umoja wa Wanafunzi Watanzania wanaosoma na kuishi Rome, ulisaidia kuhamasisha kwa nyimbo za kiswahili, zilipambwa kwa mdundo moto moto na vigelegele vya furaha, kama alama ya kushangilia matendo makuu ya Mungu kwa Kanisa Barani Afrika.
Kwaya hii iliongozwa na mtaalam wa muziki wa dini na maisha ya kiliturjia, Mheshimiwa Padre Paterni Patrisi Mangi, kutoka huko Jimboni Singida, na kwasasa akisoma Rome. Katika Taasisi ya Kipapa ya Liturjia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmi, kilichoko hapo hapo mjini Rome.
-Kwa hakika ni tukio ambalo limeacha gumzo kwa watu waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.
No comments:
Post a Comment