Saturday, November 20, 2010

MAPENZI NI AFYA, NI KILA KITU LAKINI YANA KANUNI ZAKE!


Hayahitaji papara kuamua kuhusu mwenzi wa maisha yako. Kuna fahari ya macho na kinachogusa mtima, usimwone barabarani mzuri, badi ukasema huyu ni wangu wa moyo wangu na ukakurupuka tu! unatakiwa ujadilianae na moyo wako halafu wewe na moyo wako mpate jibu linalokubalika.
Kupata mwenzi wa maisha ni sawa na Serikali ya Umoja wa Mataifa, tofauti na ile ya Zanzibar au ya Kenya, hii inahusisha maridhiano kati ya macho na moyo, macho yanaona na kuvutiwa, moyo unaguswa. Kwa mantiki hiyo ni kosa kujiaminisha kwamba unapenda ikiwa moyo haujakubali, lakini haiwezekani moyo ukapenda ikiwa macho yamekataa. Macho yanaona, ubongo unatafsiri halafu moyo unapokea. Lazima vyote hivyo vikubali na viendane sawa, hapa kuna maana kuwa umemkubali, lakini jiulize tena na tena kuhusu yeye. Kama kuna shaka ndani yake usilazimishe, badala yake pitisha uamuzi mmoja pale ambapo umeona majibu yanakuja Chanya (+) kila ulipo jiuliza. Je nipo tayari?

Binadamu hajakamilika, pengine kuna mambo ambayo yanamzunguka mwenzi wako. Watu wa pembeni wanazungumza, lakini pia si ajabu ikiwa kuna vikwazo vya Kifamilia. Jiulize kama upo tayari kukabiliana na presha za watu na ndugu ilimradi uhakikishe unambakiza kwenye himaya yako. Isitokee ukasema upo tayari leo...lakini baada ya muda ukamfanya mwenzako ajute.
Jamani tusiumizane na kutaniana katika mapenzi, kwani yanauma sana hakuna mfano, unampenda leo kesho unamwacha bila sababu...ndio maana tunasema tufikiri vizuri sana kabla ya kuanza mapenzi na mwezi. Tukumbuke mapenzi si mchezo tu, unamwacha unamrudia...kama vile kupanda daladala na kutelemka, tuache hizo.

Usithubutu kupenda kwa fahari ya jicho la leo. Nimekutaka ujadiliane na moyo wako, kwasababu kuna vitu vingi vya kujiridhisha kabla ya kuamua kuzama moja kwa moja. Ikiwa kuna dalili kwamba ipo siku utamchoka usithubutu kabisa kumpotezea muda wake.
Mwenzi wa maisha ina maana ni mtu wa furaha yako kwa maisha yako yote, kwamba yeye atakuwa sehemu ya maisha yako. Hivyo huyo hutakiwi kumchoka bali anastahili hifadhi ya kudumu moyoni mwako siku zote kuliko mwingine.

Mpenzi wako ni binadamu siyo Malaika, hivyo ndivyo na wewe ulivyo. Nyote ni viumbe dhaifu, kwa hiyo kila mmoja ana mapungufu yake, lakini kwako ni vizuri ukajiuliza endapo maudhi yake unaweza kuyavumilia.
Ruhusu moyo wako uamue katika maudhi yanayosumbua kutoka kwa mwenzi wako, moyo wako upime kwamba ubora wake upo juu kuliko kasoro zinazokutibua. Hapo unangoja nini tena? Mng'ang'anie huyo huyo, ukitaka asiye na kasoro utasubiri sana...matokeo yake huta mpata kamwe.
-GLOBAL PUBLISHERS.

No comments:

WATEMBELEAJI