Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha siku ya Ukimwi Duniani, hapo tarehe mosi Desemba, 2010 kwa wasi wasi na mashaka makubwa kutokana na ukata unaoendelea kujionyesha kwa wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya gonjwa hili la Ukimwi, kukosa fedha za kugharimia utoaji wa dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa Ukimwi.
Maambukizi ya Ukimwi bado yanaendelea kuongezeka siku hadi siku, katika kipindi cha mwaka 2008 jumla ya watu millioni moja nukta tisa waliambukizwa Virusi vya Ukimwi, kusini mwa Jangwa la Sahara na takwimu zinaonyesha kwamba; wagonjwa millioni moja nukta nne walifariki dunia kutokana na ugonjwa huu wa Ukimwi na magojwa mengine nyemelezi.
Gharama za matibabu ya dawa za kurefusha maisha, kimsingi ni mchango na mshikamano unaotolewa na wafadhili kutoka nchi za nje, ambao kwa sasa wanakabiliana na ukata mkubwa wa fedha, hali ambayo inatishia kuporomosha mafanikio yaliyokwisha kupatikana kutoka katika nchi zinazo endelea Duniani katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi. Uhaba wa dawa za kurefusha maisha ni matokeo pia ya matumizi mabaya na ukosefu wa fedha, bila kusahau athari za myumbo wa uchumi wa Kimataifa.
Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba Jumuiya ya Kimataifa inatumia rasilimali kidogo iliyopo kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa na waathirika wa Ukimwi kwa ujumla. Inasikitisha kuona kwamba; licha ya ugonjwa wa Ukimwi kuwa ni kati ya vyanzo vikuu vya vifo kwa watu wengi Duniani, lakini Jumuiya ya Kimataifa inaonyesha kuchoshwa na hali hii na kwamba Ukimwi si tena kati ya vipaumbele vyake katika huduma ya afya, jambo ambalo ni hatari katika harakati muhimu za mapambano dhidi ya baa la Ukimwi Duniani. Matokeo yake ni hukumu ya kifo kwa wagonjwa wa Ukimwi.
-Tarehe 01/12 ni siku ya Ukimwi Duniani, hudumia kwa moyo wako wote wagonjwa wa Ukimwi!
No comments:
Post a Comment