- Tunawapongeza sana wale wote wanaosimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha ya mwanadamu katika hatua zake mbalimbali, kuanzia pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida kadiri ya mpango wa Mwenyezi Mungu yanapomfika.
Maisha ya kila Mwanadamu yanathamani na utakatifu wake....na kamwe hayawezi kulinganishwa na kitu chochote kile, kwani ameumbwa; mwili na roho...anaye mapungufu yake kama sehemu ya ubinadamu wake, lakini ana uwezo wa kufanya majadiliano ya kina na Mwenyezi Mungu, Muumba wake; ili kujenga urafiki mkamilifu. Kila mtu anao wajibu na dhamana ya kulinda na kutetea tunu hii nzuri ya maisha. Ni mwaliko wa kuwa na imani na matumaini kwa mwanadamu mwenye akili na utashi, uwezo wa kufikiri na kutenda. Mtu huru katika undani wake, na kamwe si kichokoo cha majaribio ya kisayansi wala mafao ya mtu binafsi. Mwanadamu ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anayepaswa kukua na kukomaa katika utimilifu wake, akionjeshwa upendo. Lakini kwa namna ya pekee, upendo huu tuusimamie kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha, hasa kwa watoto ambao bado hawajazaliwa wale ambao kimsingi wanakabiliwa na hatari ya kutolewa mimba kutokana na ubinafsi dhamiri, pamoja na utamaduni wa kifo unaoendelea kumnyemelea mwanadamu katika hija ya maisha yake ya hapa duniani.
Utoaji mimba ni kwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu, mtu anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake; anapaswa kulindwa, kutunzwa na kupatiwa tiba msingi anayohitaji. Viinitete kadiri ya mafundisho vina uwezo mkubwa wa kuwasiliana na mama mjamzito, ni uhakika unaotolewa na tafiti za kisayansi, unaoviwezesha kukua na kukomaa na hatimaye kuwa ni kiumbe. Viinitete si mkusanyiko wa chembe za kibaiolojia, bali ni mwanadamu hai...na kama ilivyo kwa kila mwanadamu tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, anapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa kama binadamu.
Kwa majonzi makubwa kwamba; hata mara tu baada ya kuzaliwa, wanakumbana na taabu ya magumu ya maisha...wakati mwingine wanatupwa jalalani kama taka, wanakumbana na baa la njaa na umaskini, magonjwa na manyanyaso...hata kiasi cha kufikia hatua ya kunyonywa na kufanyishwa kazi ngumu, kinyume kabisa cha haki ya mtoto. Uvunjaji wa haki msingi za mtoto ni changamoto inayopaswa kugusa na kuamsha dhamiri nyofu kwa watu wote wenye mapenzi mema, ili waweze kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha.
Kila mtu ana dhamana ya kulinda, kupenda kuhudumia zawadi hii nzuri ya maisha; kama sehemu ya mchakato wa kudumisha haki, maendeleo, uhuru wa kweli, amani na furaha ya ndani. Kwa namna ya pekee tunawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa katika masuala ya kisiasa na kiuchumi, wadau wa sekta ya mawasiliano ya Jamii kuhakikisha kwamba; wanatumia uwezo wao wote kujenga msingi wa utamaduni unaoheshimu na kuthamini zawadi ya maisha, kwa kuunda mazingira ya ukarimu kwa zawadi ya maisha na ukuaji wake.
No comments:
Post a Comment