Ee Mungu Mwenyezi, asili ya kila kilicho chema...tunakushukuru kwa mema yote uliyotujalia sisi Watanzania. Tunapoadhimisha Jubilei ya miaka hamsini ya Uhuru wetu, tunakushukuru kwa kutuwezesha kuishi maisha mema kama iwastahilivyo wana wa Mungu. Kwa kutumia busara za waasisi wa Taifa letu, umetujalia tuwe Taifa moja lililounganika katika umoja, upendo, amani na mshikamano wa Kitaifa. Katika Kanisa, kwa baraka zako...umetujalia ufanisi mkubwa tunavyoshuhudia hivi leo.
Kwaajili ya mateso na kifo cha mwanao bwana wetu Yesu Kristo, tunakuomba msamaha kwa yote kabisa, ambayo kama mtu mmoja mmoja, kama Jumuiya, kama Kanisa na kama Taifa, tumeyafanya kinyume cha mapenzi yako.
Utuangazie sisi sote Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, tuwe chumvi na nuru, dira na chachu bora ya kukuza upendo, haki, uelewano, uvumilivu, mapatano, amani na umoja na hivyo uhuru wetu upate mvuto kwaajili ya wote. Uwaangazie viongozi wanaotutawala kwa niaba yako, watuongoze tuweze kukaa kwa amani na mshikamano wa Kitaifa. Sheria wanazozitunga ziwe adilifu kadiri ya mpango wako wewe uliyetuumba kwaajili yako. Bariki Taifa letu liweze kukaa kwa mapatano na mataifa mengine.
Tunaweka mbele yako changamoto nzito zinazolikabili Taifa hili na mambo yote yaliyo kinyume kabisa na mpango wako wa kutaka tuishi kwa amani, zishindwe kuathiri tunu bora ulizotujalia.
Tunawaombea Waasisi wa Uhuru huu wa nchi hii waliotutangulia...uwapumzishe kwa amani kwako mbinguni. Nasi utufadhilie kufikia ukomo uliotutayarishia wewe Mungu, wa kuwa raia katika ufalme wako Mbinguni milele yote!
Tunaomba Bikira Maria Malkia wa Amani Mwombezi na msimamizi wa Taifa letu....atuombee!
AMINA.
No comments:
Post a Comment