Wakati huu Watanzania tunapofanya kumbukumbu ya siku ya Mwalimu Nyerere, inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 14/10. Basi nasi tunasema; Mwalimu Nyerere ni muasisi wa Taifa letu huru la Tanzania, mfano bora wa kuigwa kutokana na ujasiri wake wa kuthubutu kwa dhati kabisa kuonesha karama na vipaji vyake alivyotumia kwaajili ya mafao ya wengi.
Mwalimu Nyerere katika hija ya maisha yake....alijitahidi kutanguliza maslahi ya watu wake bila ya kujikita katika ubinafsi, uroho na uchu wamadaraka. Uchoyo na ubinafsi; dhambi zinazoendelea kuwatesa sana viongozi wengi Barani Afrika. Katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika, Mwalimu alipiga moyo konde kwa kusonga mbele kwa ujasiri mkubwa licha ya vikwazo na matatizo alivyokuwa anakumbana navyo hadi Tanganyika ikapata uhuru wake wa bendera kwa njia ya amani.
Kama kiongozi alikuwa na dira, ndoto, sera na vipaumbele vya Taifa, mintarafu mazingira ya wakati wake, daima alipania kuwaletea Watanzania maendeleo ya haraka katika sekta mbalimbali za maisha. Baadhi ya vipaumbele hivi ni; Umoja wa Kitaifa, Haki, Amani, Usawa na Maendeleo kwa wote.
Pengine kutokana na mwono na maelekeo ya sasa baadhi ya sera na vipaumbele vinaweza kuonekana kana kwamba; vilikuwa na mapungufu, lakini daima ikumbukwe historia na nia kubwa ya Mwalimu Nyerere ya kutaka kuwaletea Watanzania wote maendeleo ya haraka bila kujali; dini, kabila, uwezo wa watu kiuchumi na kijamii. Alitamani kuiona Tanzania inakuwa ni kati ya nchi ambazo zinacharuka kwa huduma za kijamii na maendeleo ya viwanda na miundombinu, kwa kuzingatia tija, ubora na viwango.
Mwalimu alikuwa na ujasiri wa kuthubutu na ndoto ya mafao ya wengi akijikita zaidi na zaidi katika maisha adili na manyofu.
Mwalimu alipenda kukosoa na kujikosoa ili kuboresha malengo na ndoto zake kwaajili ya mafao ya wengi nchini Tanzania. Mapungufu yaliyojitokeza katika kusimamia na kutekeleza sera na mipango ya Kitaifa, isiwe ni hoja ya msingi inayofuata matendo makuu ambayo Mwalimu Nyerere amewafanyia Watanzania na Waafrika wakati wa uhai wake. Kama binadamu alikuwa na karama pamoja na utajiri mkubwa wa kimawazo aliokuwa amekirimiwa na Mwenyezi Mungu, lakini pia alikuwa na mapungufu yake; kama tulivyo sisi sote binadamu wa ulimwengu huu.
Ndoto, Dira, Malengo na vipaumbele vya Mwalimu; bado ni hai na endelevu kabisa, ikiwa kama vitaboreshwa na kudumishwa kwa kusoma alama za nyakati, kama njia sahihi ya kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere....katika yale aliyosimamia kwa dhati kabisa kama vipaumbele vya Kitaifa.
No comments:
Post a Comment