.........MARADUFU NA HIVYO KWAFANYA WATU WENGI ZAIDI KUOGELEA KATIKA DIMBWI LA NJAA, UMASKINI NA UTAPIAMLO!
Taarifa ya hali ya usalama wa chakula kwa mwaka 2011, iliyotolewa na Mashirika ya chakula na kilimo ya Umoja wa Mataifa inaonesha kwamba; bei ya chakula itaendelea kupanda maradufu, hali itakayofanya wakulima,walaji na wananchi kutoka katika nchi zinazoendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini na baa la njaa. Nchi za Kiafrika ambazo kwa kiasi kikubwa zinategemea kujitosheleza kwa kuagiza chakula nje ya nchi zitaathirika zaidi na mfumuko wa bei ya mazao ya chakula duniani. Hizi ni nchi ambazo bado zinaendelea pia kuathirika na myumbo wa uchumi Kimataifa uliojionyesha kwa namna ya pekee kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2008.
Baa la njaa na ukame unaoendelea kuzikumba nchi zilizoko kwenye pembe ya Afrika ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika harakati za kupunguza kwa kiwango, watu wanaoathirika kwa baa la njaa kama sehemu ya mbinu mkakati wa malengo ya maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015 zinaonekana kugonga mwamba. Ni onyo ambalo limetolewa na wakuu wa Mashirika ya chakula na maendeleo ya kilimo ya Umoja wa Mataifa katika utangulizi wa taarifa hii. Tatizo la utapia mlo bado linaendelea kutesa watu wapatao millioni mia sita wanaoishi katika nchi zinazoendelea duniani, jambo ambalo haliwezi kukubalika ki maadili, ingawa ndio ukweli wa mambo ulivyo. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati, ili kuhakikisha kwamba baa la njaa na utapia mlo linatokomezwa kutoka katika uso wa dunia. Serikali mbalimbali kwa upande wake zinapaswa kuongozwa na sera za uwazi na ukweli, kwa kujenga mazingira bora zaidi ya uwekezaji unaofanywa na sekta binafsi na wakulima wadogo wadogo ili kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo. Kuna haja pia kwa nchi zilizoendelea kuwa na matumizi mazuri zaidi ya chakula, sanjari na kuongeza jitihada za uzalishaji katika nchi zinazoendelea, kwa kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali; hifadhi ya misitu na uvuvi bora zaidi...ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani.
Kuna haja ya kuwa na mipango ya muda mrefu na mfupi katika maswala ya kilimo, jambo ambalo limekuwa likizungumzwa na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Kimataifa, lakini matokeo yake bao hayajaonekana kuwa yanatia moyo. Kilimo cha umwagiliaji, matumizi bora ya ardhi, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, mbegu bora na tafiti zinazolenga kuboresha tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika mkakati wa kuwa na usalama wa chakula duniani. Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa linakadiria kwamba; kuna jumla ya watu millioni mia tisa na ishirini na tano walioathirika na baa la njaa kwa mwaka 2010, ikilinganishwa na watu millioni mia nane na hamsini waliokuwa wameathirika katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2008. Idadi ya waathirika wa baa la njaa kwa mwaka 2011 bado inaendelea kufanyiwa kazi na FAO.
No comments:
Post a Comment