Monday, March 26, 2012

WAKULIMA WADOGO WADOGO WAKIWEZESHWA WANAWEZA!

WAKULIMA WADOGO WADOGO WAKIWEZESHWA....WANAWEZA KULETA MABADILIKO MAKUBWA KATIKA SEKTA YA KILIMO!


Kwa miaka mingi kilimo hakikupewa msukumo wa pekee, hali ambayo imewapelekea wakulima wengi kujikuta wakiogelea katika dimbwi la umaskini, hali inayowalazimisha kutoa ardhi yao kwa wawekezaji wakubwa kwa bei ndogo kabisa. Wakulima wadogo wadogo pia wamekuwa hawana uhakika wa soko la mazao yao, sanjari na miundo mbinu mibovu...mambo ambayo yamesababisha pia ongezeko la baa la njaa duniani.
Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwawezesha wakulima wadogo wadogo kuwa na uhakika wa soko la mazao yao; Serikali kwa upande wake zinapaswa kutekeleza majukumu yake kimsingi, ili kuhakikisha kwamba; wakulima wanafaidika na jasho lao......badala ya kuendekeza mtindo wa sasa unaotoa faida kubwa kwa walanguzi wa mazao ya wakulima hasa Vijijini.

Wakulima wadogo wadogo wanapaswa pia kuwezeshwa ili kupata haki katika mauzo ya ardhi yanayoendelea kufanyika sehemu mbalimbali hasa katika nchi maskini duniani. Wakulima hawa wanaathirika sana wakati wa mfumko wa bei ya mazao ya chakula kwenye soko la Kimataifa, lakini kwa bahati mbaya hawana sauti. Ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuwajengea uwezo wakulima, kuna haja ya kuhakikisha kwamba; wanaboresha mazao ili kupata walau bei nzuri katika soko la Kimataifa, baadhi ya maeneo yatengewe rasmi kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula, vinginevyo baa la njaa litaendelea kuwa ni wimbo uliozoeleka maskioni mwa watu.

Jamii iwawezeshe Wanawake katika maamuzi yanayohusu masuala ya mazao ya biashara na chakula, kwani; kuna hatari kwa mfumo dume kutawala katika masuala ya mazao ya biashara, kwani wao ndio wanaofaidika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na Wanawake. Masuala haya yasipozingatiwa kuna hatari kwamba; hali ya usalama wa chakula itakuwa daima mashakani na wakulima wenyewe wataendelea kuogelea katika umaskini na madeni makubwa. Serikali zina wajibu wa kuhakikisha kwamba, wakulima wanapata kwanza kabisa; ujuzi na maarifa ya kilimo bora na cha kisasa, huduma za pembejeo za kilimo na habari muhimu kuhusu mwenendo wa soko la mazao yao. Wakulima wadogo wadogo wahamasishwe kuunda vyama vya ushirika vitakavyo simamia mchakato mzima wa shughuli za kilimo; soko na bei halali ya mazao yao.

Mahali ambapo vyama vya Ushirika vimetekeleza majukumu yake kwa ufanisi na uwajibikaji mkubwa, hapo wakulima wameweza kufaidi jasho la kazi yao. Lakini kwa bahati mbaya uzoefu na historia imeonesha kwamba; kuna baadhi ya wajanja wachache katika vyama vya Ushirika wanaofaidi jasho la wakulima. Ikumbukwe kwamba; wakulima wadogo wadogo wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo, ikiwa kama watawezeshwa kikamilifu.

No comments:

WATEMBELEAJI