......WANASAYANSI JIKITENI KATIKA MISINGI YA MAADILI, UTU WEMA NA MAFAO YA WENGI KATIKA TAFITI ZENU.
Tunaweza kuzungumzia masuala nyeti ndani ya Jamii, hasa madhara ya utoaji mimba jinsi ambazo wanawake ambao wamefanya tendo hilo, wanavyoendelea kusutwa na dhamiri nyofu...baada ya kutema zawadi ya uhai.
Tukumbushane umuhimu wa dhamiri nyofu kwa kutambua kwamba; dhamiri ni hukumu ya akili ambayo mwanadamu hutambua sifa adilifu ya tendo halisi analoelekea kulitenda. Katika yote asemayo na atendayo, mwanadamu hana budi kufuata kiaminifu anachojua kuwa ni haki na sahihi.
Dhamiri ni sheria ya Mungu iliyoandikwa katika moyo wa mwanadamu na wala si dhana inayopatikana kwa wakristo au waumini peke yao ni urithi wa kila mwanadamu. Hapa ni mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anaongea na mtu kutoka katika undani wa maisha yake na kumpatia changamoto ya kulinda na kutetea zawadi hii ya maisha katika hatua zake msingi za ukuaji na utekelezaji wa mwanadamu, ndio daraja msingi kati ya Mungu na mwanadamu, unaotoa uzito wa pekee katika dhamiri maadili.
Dhamiri ni kiashilia cha akili, vionjo na utashi wa mtu kumwilisha ndani mwake kile kilicho chema cha kufuata na jambo baya ili kuliepuka, kwani uamuzi wowote utakaochukuliwa na mtu unaacha chapa ya kudumu katika maisha yake. Anapata mahangaiko ya ndani, ikiwa kama anakwenda kinyume na dhamiri yake nyofu, lakini hata katika hali kama hii Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuzungumza naye katika dhamiri fuatizi, ili kutambua kosa lililotendwa na kuomba huruma ya Mungu, ili kuponya majeraha haya.
Tunawaalika Madaktari kusimama kidete kulinda na kutetea dhamiri nyofu za wanawake, wanaokimbilia kwao wakitaka kutoa mimba, kwamba; kutambua madhara watakayokumbana nayo katika familia, uchumi, jamii na afya ya watoto wao. Wakati mwingine Madaktari wamewalazimisha wanawake kutoa mimba kwa kisingizio kwamba; ni kwa ajili ya mafao ya afya ya mtoto na familia yake na kwamba; atakuwa mzigo kwa jamii yake. Changamoto hii ni kulinda na kutetea utamaduni wa maisha.
Napenda kuchukua fursa hii kuialika Jamii nzima kujenga utamaduni wa kulinda na kutetea zawadi hii nzuri ya maisha...tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, na mafao ya wanawake wenyewe badala ya kukimbilia falsafa ya utoaji mimba. Jamii iwasaidie wanawake ambao wamejikuta wakilazimika kutoa mimba, wasaidiwe kwa njia ya mshikamano wa upendo. Wawe daima ni watu wamatumaini na kamwe wasikate tamaa, wasimamie ukweli na kuomba msamaha wa dhati kutoka katika undani wa mioyo yao, kwani Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, anawasubiri katika kiti cha maungamo ili kuwaonjesha upendo na huruma yake isiyokuwa na kifani. Lengo ni kuwawezesha wanawake waliotoa mimba kuwa ni mashaidi na watetezi wa zawadi hii nzuri ya uhai.
Hata watafiti wa masuala ya viini tete wanahusika kikamilifu kwa kutambua kwamba; wanao mchango mkubwa katika tiba ya mwanadamu ndani ya Jamii, changamoto ya kuzingatia maadili, tunu ya mshikamano wa dhati na daima wawe mstari wa mbele kutafuta mafao ya wengi. Tunawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema; kwa namna ya pekee kutambua umuhimu wa mshikamano wa kiutu. Nasi tutaendelea kuheshimu tafiti za kisayansi zinazofanywa na wanasayansi kwa kutingatia misingi ya kimaadili katika utekelezaji wa majukumu yao, kwaajili ya mafao ya binadamu. Ni matumaini yetu kwamba; wataalam katika masuala ya tiba na maisha ya mwanadamu wataendelea kutekeleza huduma yao kwa kutambua na kuthamini mahitaji msingi ya kiroho na kimwili.
No comments:
Post a Comment