Monday, April 4, 2011

FAMILIA NI KITALU CHA MALEZI YA VIJANA!

Familia ni mahali ambapo umoja, mshikamano na huruma hukuzwa na kuendelezwa kwaajili ya mafao ya wengi. Ni mahali ambapo Jumuiya ya watu hujengeka na kukua, mshikamano wa maisha ya kifamilia ni kigezo cha ubora wa maisha ya Kijamii. Familia ni mahali pa zuri kwa yote mazuri, na ni shule kubwa sana katika kukuza vijana; wazazi ni walimu wa kwanza wa watoto wao kwa kushirikiana kikamilifu na wadau mbalimbali katika malezi na makuzi ya watoto wao.

Tuchambue mada hii kwa mapana, mintarafu changamoto kuhusu malezi ya vijana wa kizazi kipya. Kwa fafanuzi zazidi nakusubiri mpendwa kijana katika makala yetu ya leo ambayo inatupia jicho tena umuhimu wa familia katika malezi ya vijana; kama changamoto kwa uhusiano unaopaswa kuwepo baina ya familia na makuzi ya vijana katika nyanja mbalimbali. Ni muhimu kuzingatia malezi ya kweli katika Jamii yetu ambamo inajidhihirisha wazi kuwa kutambua misingi ya maadili peke yake hakutoshi. hali kadharika hata elimu itolewayo na Jamii bado haijitoshelezi katika kuwajenga vijana kwani; imegubikwa sana na maandalizi ya kitaaluma na matumizi ya muda fulani tu katika maisha. Kuna haja yakuwa na uhusiano wa kweli kati ya shughuli tufanyazo na malezi ya kila siku yaliyojengwa katika uhuru wa kweli na mahusiano ya kweli.
Tunasisitiza umuhimu wa kila anayehusika na maandalizi ya vijana kwa ajili ya maisha yao ya baadaye, kuzingatia malezi yanayolenga katika kumwezesha kijana kutekeleza wajibu wake wa kila siku kwaajili ya kujenga Jamii yenye misingi yake katika upendo wa kweli na uwajibikaji wa kweli. Uhusiano huu ambao ni wa muhimu sana kati ya kijana na Jamii yake, ndio msingi wa mabadiliko yoyote ya kweli.
Familia zinawajibu wa kutambua nafasi yao ya kipekee katika kutoa mwelekeo unaofaa kwa maisha ya baadaye ya kijana. Hii ni elimu ya kwanza kabisa ambayo kila binadamu mkamilifu anapaswa kuwa nayo. Ni misingi ambapo patajengwa utambuzi mwingine wote unaotolewa na elimu ya kisayansi na teknolojia. Kwa hali hiyo familia zinapaswa kuzingatia ukweli kwamba; sura ya mtu inayojionyesha katika Jamii inawakilisha elimu ya malezi ya familia husika.
Kwa bahati mbaya, maendeleo ya kisayansi na teknolijia yamekuwa yakiingilia kwa kasi kubwa sana tunu hii ya malezi. Kutokana na kuvurugika huku kwa malezi katika familia ndipo tunakutana na miyumbo ambayo inajidhihirisha sasa katika masuala ya kiimani.

Makala yetu hii inawaalika wanafamilia wote kutafakari ukweli mzito uliomo katika maneno haya yote tulio yaongelea na kuzingatia umuhimu wake kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

1 comment:

Mama Pam Augusta said...

NIMELIPENDA SOMO HILI ASANTE SANA BARAKA.UTAKUWA BABA MWEMA SANA ALL THE BEST ALWAYS.

WATEMBELEAJI