Thursday, January 26, 2012
WAZIRI MKUU PINDA, ASEMA; WANAOTAKA URAIS HAWAUJUI.
''WANAOUTAKA URAIS HAWAUJUI...URAIS NI KITU GANI'';
Hii ni kauli aliyotoa jana Waziri Mkuu, Mh.Mizengo Pinda, Dar es salaam....alipoulizwa kama atawania Urais wa Tanzania ifikapo Mwaka 2015.
''Haiwezekani mtu ukautaka Urais, isipokuwa kama hujui ni nini Urais au pengine unafuata maslahi'' alisema hivi Pinda.
Waziri Mkuu Pinda, alikuwa akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu mambo mbalimbali yaliyojiri nchini katika kipindi cha miezi sita iliyopita. Kabla hajasema hayo, alikanusha akisema; hagombei na wala hatanii kwa hilo, akisema ifikapo Mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 67, hivyo akigombea akashinda atakuwa na miaka 5 zaidi na atakuwa amezeeka.
Wanaotaka Urais waendelee nao, lakini mimi naona hapa (Ikulu) ni kazi ngumu kwasababu hulali......napajua hapa, nimetumia sehemu kubwa ya maisha yangu ya utumishi nikiwa Ikulu. Nilianza na Mwalimu Nyerere, akaja Mwinyi, kisha Mzee Mkapa.....nilipoachana nao nikaingizwa kwenye siasa, nilipoambiwa eh bwana njoo huku.....nimechangia vya kutosha na sasa nitapumzika.
Alisema; Mungu aliumba Binadamu wafanye kazi, lakini pia wapate muda wa kupumzika. Pinda alisema; ameshatoa msimamo wake huko nyuma na jana akarudia ili ueleweke, ingawa alisema watu wengine wakimsikia anasema hivyo, wanaweza kumshangaa na kumwuliza kwanini aseme hayo.
Alisema; anamhurumia sana Rais Jakaya Kikwete, kwa kazi kubwa anayoifanya na kila akienda kumwona anamwambia ni kazi nzito Ikulu.
Alitoa mfano siku Rais Nyerere anang'atuka, alipotoka Uwanja wa Taifa kuagwa rasmi, ''alifika nyumbani akapanda juu, mimi nilikuwa pale...tukiwa vijana wakati huo (1985) alipoteremka akamwambia msaidizi wake; Joan Wickens (Marehemu) kwamba; anajisikia faraja kama mtu aliyeondolewa na kitu fulani mwilini. Alionekana kama katua mzigo mzito uliyokuwa unamwelemea.....hii ni kazi nzito si ya kuitaka, labda Wananchi wenyewe ndio wakutake uwe Rais, lakini si kuikimbilia.
Kauli hiyo inafanana na aliyopata kuitoa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Mwaka 1995 kwamba; Ikulu si mahali pa kukimbilia, kwasababu ni mzigo mzito sana!
- Habari na Joseph Kulangwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment