Pale furaha ya kwenda Majuu kula kuku kwa mrija, inapogeuka kuwa kunywa soda kwa uma. Sulubu, majonzi na majuto vikiwa ndizo hali za kila siku, kwa mtu aliyeingia katika mtego huo.....wa kupelekwa majuu, basi hili linakuwa ni tatizo la kijamii linalo hitaji kupata jibu linalofaa. Tatizo hili la watu kusafirishwa kutoka maeneo yao hadi sehemu nyingine kwa ahadi za uongo za kupata kazi....watu wanaojikuta wameingia bila kujua katika mazingira magumu, ya kufanyishwa kazi kama watumwa kwa ahadi za uongo zinazotolewa na watu fidhuli wanaotafuta utajiri wa haraka haraka tu, kwa kuwauza kiujanja binadamu wenzao.
Kwanza kabisa kuna aina mbili za watu kuingia katika utumwa mambo leo bila ya kujijua, watu wazima na hata watoto. Wanaokuwa kafara zaidi katika biashara hii haramu hasa ni vijana mwenye umri wa kati wale wanaopevuka kuingia kundi la watu wazima wake kwa waume. Na hasa wale ambao kiwango chao cha elimu rasmi kiko chini, wanaotoka katika familia fukara, wenye hamu ya kupata kazi kwa haraka kwaajili ya kujipatia riziki kwa wao wenyewe na hata fedha za kutosha kukimu maisha na kuboresha hali yao ya maisha kwao wenyewe na pia kwa ajili ya familia zao. Bahati mbaya ya watu wenye uchu wa kupata utajiri wa haraka haraka, wadhalimu wasiojali utu wa wengine, huuchukulia unyonge wa wale wanaotafuta kuboresha maisha, kwa vishawishi vya uongo wakiwa bado katika mazingira ya nyumbani kwao. Ahadi za kupata kazi nzuri na hivyo maisha kubadilika kuwa mazuri zaidi mbali na maeneo yao mahali na hasa kwenda Majuu kama Ulaya, kinakuwa ni kivutio kikali cha kuwaingiza wanyonge katika mtego huu.....mara nyingi kazi hizo wanazoahidiwa huwa hazipo. Mara wanapowasili walipo ahidiwa kupata kazi, kafara hunyang'anywa hati zao za kusafiria na waajili hao dhalimu.....mtu hujikuta akipewa kazi tofauti na ile aliyo ahidiwa akiwa nyumbani kwao. Wasichana hulazimishwa kuolewa, kufanya ukahaba, kazi za ndani, kuombaomba, kuburudisha katika vilabu vya pombe na hasa usiku, au kufanya kazi kwenye mahoteli na mabaa kama wahudumu na kadhalika bila hiyari yao. Mbaya zaidi wengine hulazimishwa hata kuwa wakala wakusambaza dawa haramu za kulevya, au kuwa walinzi katika makampuni binafsi.
Kafara; wote hao huwa na hali za kufanana, kama mishahara midogo sana au kutolipwa kabisa....wengi hubaki wamefungiwa majumbani na baadhi hupata adhabu za kusulubu mwili kama kupigwa na kuwekwa katika hali ya mfungwa kabisa katika majumba binafsi, kubakwa na kushindishwa njaa. Wanafichwa na kuzuiwa kukutana na watu......na mara nyingi hupewa vitisho vya kuuawa iwapo watagundulika kuwa na mawasiliano na watu wa nje. Matokeo yake hawana mahusiano ya moja kwa moja na watu wengine na hivyo hujawa nahofu, masononeko na mifadhaiko daima wakiwa na woga wa kujieleza kwa vyombo vya usalama kama; Polisi. Wengi hubaki katika hali hizo kwa muda mrefu na hata miaka mingi, wewe mzazi upo huko nyumbani unasema mtoto wako yupo Majuu bila wasiwasi, kumbe anapata tabu sana tena sana!
Kwa upande wa watoto mara nyingi wa kulaumiwa ni wazazi au jamaa zao wanaowauza kwa watu dhalimu. Wazazi na Jamaa zao hushawishika kwamba; watu hao wataweza kuwatunza watoto katika hali nzuri na salama kwa maisha mazuri.....lakini kumbe mara wakiwa katika mikono ya dhalimu, utu wao na haki yao kama watoto huvuliwa na kuanza kufanyishwa kazi kwa nguvu hasa kazi za ndani majumbani, na wengine huingizwa katika biashara haramu ya ukahaba na kuwa watumwa wa ngono.....mbaya zaidi fedha wanazolipwa katika vitendo hivyo viovu si mali yao, lakini huziwasilisha zote kwa mabwana hao. Na kuna wengine wanao fanyishwa kazi za sulubu au kusajiriwa kama Maaskari wapiganaji......katika hali na mazingira hayo, yeyote anayejishughulisha na udhalimu huu hana tofauti na wale waliofanya biashara ya utumwa karne za nyuma, kwa kuwa utendaji wake ni sawa sawa na ilivyokuwa wakati wa utumwa.
- Hivyo natoa wito kwa wote; Wazizi, Walezi na Wana Jamii kwa ujumla, kuwa makini na jambo hili, hasa kwa vijana walio wengi kutaka kwenda Majuu bila mpangilio wowote. Usindanganyike kirahisi rahisi....utajikuta maisha yako yanabadilika kuwa mabaya zaidi ya hapo ulipo kwasasa. Shida zako na ndoto zako za kwenda Majuu, zisikufanye ukurupuke kwa jambo hili....jipange vizuri na uende kwa uhakika zaidi, sio kukurupuka tu na kudanganyika ki urahisi rahisi tu!
No comments:
Post a Comment