DHAMANA YA VIJANA NA MAENDELEO YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA YA HABARI!
Kuna upepo mkali wa mabadiliko ya kijamii unaoendelea kuzikumba nchi mbalimbali Barani Afrika, anayedhani kwamba; amesimama ajiangalie asianguke. Maneno ya burasa kutoka kwa wahenga wetu Barani Afrika. Mabadiliko haya ni matunda ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, mwamko na hatua mpya ya vijana kutaka mabadiliko katika medani mbalimbali za maisha ya kijamii, lakini kwa bahati mbaya mabadiliko jamii yanaendana na umwagaji wa damu ya watu wasio na hatia. tunauangalia upepo huu kwa jicho la makini zaidi na kutoa angalisho kwa vijana kutotumiwa na wanasiasa kama vyombo vya kuleta machafuko ya kisiasa.
Mpendwa sana kijana, tabia ya mabadiliko katika ulimwengu wetu huu si suala la kuumiza vichwa. Tangu kuumbwa kwake Dunia imekuwa ikipitia vipimo mbalimbali vya mabadiliko ambayo kila yatokeapo mara nyingine huamsha hisia fulani katika maisha ya mwanadamu. Hali kadhalika mabadiliko kama vile ya kimsimu; mvua, jua, theruji, masika na kiangazi, yanaendelea kila mwaka na kufika hali ya kuzoeleka kiasi kwamba yanapokosekana kila kiumbe juu ya uso wa nchi huingia wasiwasi, huzuni na mashaka si tu kuelekea mabadiliko husika bali hasa katika kuhofia maisha yake ya kesho.
Bado hata katika tabia ya nchi namna ya mabadiliko ya kawaida hutofautiana kulingana na jinsi yanavyotokea. Kwa mfano mvua ni mvua, lakini mvua hupata jina kutokana na jinsi inavyoshuka katika uso wa dunia hii. Kuna dhoruba, kuna manyunyu, kuna masika nk. Bado pamoja na mabadiliko ya sifa hizi, mvua inabaki kuwa mvua tu.
Ikiwa sio nia yangu kuzungumzia tabia ya nchi, napenda sana kuangalia mabadiliko katika hali ya kijamii na hasa inapomgusa binadamu, bwana wa mabadiliko haya. Ni wazi katika kusema binadamu sina maana ya kuukataa ukweli kwamba katika kuleta mabadiliko ya kijamii, mazingira, mali na hata wanyama wanaonja manufaa haya, daima sambamba na binadamu bwana wa mabadiliko ya kijamii. Hali hii si hadithi katika dunia yetu hii ya leo, mabadiliko ya kijamii yamekuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku kama vile kuchomoza na kuzama kwa jua. Bado hali hii ina umuhimu wake katika kumkamilisha binadamu, kinachoshangaza na kuyapa majina mbalimbali mabadiliko haya ni uwajabu wake, na wakati mwingine ulimbukeni tu! Kama vile mvua inavyoweza kubadilika toka manyunyu na kuwa dhoruba, mabadiliko ya kijamii yanaendelea kuwa tishio kwa binadamu, bwana wa mabadiliko haya. Upoteaji wa maisha na umwagikaji wa damu umechukua sura ya mabadiliko katika jamii ya binadamu sehemu mbalimbali duniani. Pengine tunatupia macho tu sehemu zile ambazo risasi na mabomu yanarindima kila sekunde, lakini hatuna budi kuangalia mfumo mzima wa jamii unaoendelea kumnyima binadamu furaha ya mabadiliko katika jamii, na ambayo vurugu na mauaji ni matokeo yake tu! Mabadiliko ya kile tunachoweza kukiita ''tabia ya nchi ya kijamii'' ni ishara ya kuchoshwa na uharibifu unaoendelea katika maisha ya kijamii sehemu mbalimbali duniani. Tabia kama vile ulaji rushwa bila woga wala huruma, ukiukaji wa haki za kidemokrasia na haki zote msingi za binadamu, ni sawa kabisa na uharibifu unaoendelea wa mazingira ya kidunia.
Wakati uharibifu wa mazingira unaishia katika kuvuruga mfumo mzima wa tabia ya nchi, uangamizaji wa haki za binadamu una matokeo yale yale ya dhoruba na vimbunga kama tunavyo shuhudia leo. Kama vile dhoruba na ukame unaotokana na uharibifu wa mazingira unavyoitesa dunia yenyewe, hali kadharika tabia za kukalia na kunyonya haki msingi za binadamu zinaendelea kummaliza binadamu mwenyewe, bwana wa mabadiliko.
Katika yote haya kijana amekuwa mwathirika wa kwanza kabisa kwani ndiye uso hasa wa jamii, na bado kijana anaendelea kulaumiwa kama si kupuuzwa katika malalamiko yake ya kukosewa haki kama vile ya elimu, ajira na hata ya maisha. Nyuma ya matatizo yote haya kumejaa mabwana wanaofaidika kutokana na kuharibu mazingira ya kijamii kwa kufyeka miti ya kiuchumi, kidemokrasia na hata ya kimaadili kila kukicha kama mchoma mkaa au muuza mbao anavyofurahia kifo cha miti bila kuangalia usalama wa tabia ya nchi.
Makala hii inalaani tabia zote zinazopelekea kuharibu amani na utulivu Duniani. Ikiomba pia kuheshimiwa kwa tabia ya asili ya kupokea mabadiliko ya kijamii, inapenda pia kuwaalika vijana wote kuepuka kutumika kama vyombo vya vurugu na umwagaji damu....unaoendelea sehemu mbalimbali duniani.
No comments:
Post a Comment