Tuesday, May 31, 2011

WAJIBU WA KILA MWANA JAMII KUKAZANIA MAFAO YA WOTE!

Jamii yoyote iliyo na ustaarabu na yenye misingi ya imani kwa Mungu, inapaswa kuona umuhimu wa kujali haki za msingi za mwanadamu, haki ambazo zinajengwa katika mshikamano wenye kujali manufaa ya wote. Kwani hitaji la manufaa kwa wote linategemea hali ya Jamii kwa kila kipindi cha kihistoria na iliyounganika kabisa kwa kuzingatia kumwinua na kumkuza binadamu kwa ujumla na haki zake za msingi. Historia makini inamsaidia mwanajamii na Jamii; kujitambua anatoka wapi, yuko wapi na anaelekea wapi katika safari yake nzima ya kufikia malengo yake ya hapa duniani na hata ya baadaye, yaani maisha ya kiroho.
Ni wito kwa kila mwanajamii kutambua kuwa yeye ni sehemu muhimu katika kutimiza hitaji hili, kuiishi imani yake kikamilifu, kimsingi; dini zote zinatambua kwamba umoja na mshikamano, ni chanzo cha haki kwa wote ni mwanzo wa kuelekea imani ya kweli inayozingatia manufaa ya wote, japo wakati mwingine upo upotoshaji wa makusudi. Na kwamba mwanajamii ana wajibu wa kuchagua na kusaidia uwepo wa Serikali makini yenye kujali manufaa ya wote, kwa kusaidia uwepo wa sheria zinazojali na kuzingatia usawa wa binadamu. Mtu binafsi bado ana nafasi ya kusaidia uwepo wa muundo thabiti wa kisheria unasaidia upatikanaji wa huduma za lazima kwa wote, ambazo kwa waati huohuo ni haki za binadamu, huduma kama; chakula, maladhi, ajira, elimu na kujali na kuziheshimu tamaduni za wengine, usafiri wa uhakika, afya bora, mawasiliano na kulinda uhuru wa dini.


Ni kweli kwamba manufaa kwa wote ni suala linalohusu na kugusa Jamii nzima, hakuna anayepaswa kulikwepa hili, ushirikiano wa kila mmoja kadiri inavyowezekana unahitajika katika kufikia na kuendeleza malengo mazima ya kuwa na Jamii yenye haki na amani. Manufaa kwa wote lazima yahudumiwe katika utimilifu wake, na siyo kwa mtazamo nusunusu unaoongozwa na watu waliouweka kwa faida yao binafsi, lazima itegemee mantiki inayochukulia uwajibikaji mkubwa na kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Manufaa kwa wote inaendana na silika za juu kabisa za binadamu, lakini ukweli kwamba ni tunda ambalo ni vigumu kulifikia kwasababu wakati wote unahitajika uwezo wa kudumu na nguvu ya katafuta manufaa ya wengine kama vile ni manufaa ya mtu mwenyewe binafsi, ni vigumu sana kwasababu sisi binadamu tunaounda Jamii daima tunakuwa na hulka ya kupenda zaidi ubinafsi, tunapenda kustawi binafsi kuliko wengine.

Tukiangalia hali halisi ya Jamii zetu na dunia kwa ujumla, tutatambua kwamba tuna mambo mengi ambayo yangeweza kutimiza mahitaji yote ya lazima ya binadamu kama tungejali manufaa kwa wote. Kwa mtazamo wangu binafsi ni kuwa; dunia ya leo haina njaa ya chakula...ila ina njaa ya upendo na mshikamano, ndio maana wakati wengine wanakufa kwa njaa ya chakula, wengine wanamwaga na kutupa ovyo chakula kwasababu hawana hitaji na wala hawana mahali pa kuweka, wakati wengine wanakufaa njaa ya chakula wengine wanaishi maisha yenye starehe za kupindukia. Hivi ndivyo wanadamu tulivyo, au tunamwelekeo huo wa kujijali na kupuuza mahitaji ya wengine hata kama wanakufa. Kila mtu katika Jamii ana haki ya kufurahia maisha ya Jamii, na hii linawezekana tu kama manufaa kwa wote yatazingatiwa. Tuna kila sababu ya kuungana kwa pamoja kwa umoja katika maswala haya muhimu ya maisha kwa wote katika haki sawa.
Mgawanyo wa mali zilizozalishwa lazima uwe wa haki, wala usifanyike katika hali ya uovu kama tunavyoshuhudia katika wakati wetu huu, ambapo pengo kati ya walionacho na wasionacho inaongezeka siku hadi siku, na kuwa pengo kubwa sana na la kutisha. Huko ni kukosa utu, haiwezekani mtu kujijali yeye tu au pengine na familia yake, wakati walio wengi wanateseka kwa umaskini uliokithiri, wewe una zaidi na zaidi lakini hutaki kutoa hata kidogo kusaidia hawa wasio nacho, kwasababu ya ubinafsi umekujaa sana. Leo katika Bara letu la Afrika umaskini unazidi kukithiri kwa wananchi wa kawaida, lakini walio madarakani wanazidi kuneemeka kila kukicha, na sababu msingi ni kupuuza maadili ya uongozi, maadili katika Jamii na hata ubinafsi. Haiwezekani kabisa kwa utajili wa maliasili tulizonazo tunaendelea kuwa maskini kila kukicha, jamani tukubali mwaliko huu; kuhusu Jamii ya kujali wote bila ya ubaguzi na kutumia yote kwa faida ya wote yaani manufaa kwa wote.

No comments:

WATEMBELEAJI