Monday, November 28, 2011

KARDINALI POLYCARP PENGO ASEMA:........

AJALI BARABARANI NI CHANZO CHA VIFO NA UHARIBIFU MKUBWA WA MIUNDO MBINU; UMEFIKA WAKATI SASA WA KULIPATIA TATIZO HILI UFUMBUZI WA KUDUMU!


Cardinali Polycarp Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameishauri Serikali ya Tanzania kuchukua hatua za makusudi kabisa ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi yanayoendelea kupukutika kutokana na ajali barabarani. Ajali hizi zimekuwa ni chanzo kikuu cha upotevu wa maisha na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu.
Kardinali Pengo aliyasema haya hapo jana tarehe 27 Novemba 2011, Jumapili jioni....wakati akiongoza Ibada ya Misa Takatifu kwaajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Mapadri; Silverio Ghelli, Padre Corrado Trivelli, Padre Luciano Baffigi, pamoja na kijana Andrea Ferri, waliofariki kwa ajali ya gari iliyotokea Ruvu kwa Zoka, tarehe 22 Novemba 2011, wakati wakitoka Dodoma kwa shughuli za kichungaji.

Kardinali Pengo anasema; ajali iliyosababisha vifo vya ndugu Wafranciskani Wakapuchini si ya mwisho na kwamba; ajali hizi zitaendelea Kuwa ni chanzo cha vifo vya Watanzania wengi, changamoto kwa Serikali na watumiaji wa barabara kuchukua hatua madhubuti ili kudhibiti matukio haya yanayoongezeka kwa kasi nchini Tanzania, hasa kutokana na kuboreka kwa barabara nyingi. Amesema; Mapadri hao wamefariki wakiwa katika huduma, mbegu safi machoni pa Mwenyezi Mungu.
Viongozi mbalimbali wa Kidini waliohudhulia Ibada ya Misa, wamelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba; sheria za usalama barabarani zinashika mkondo wake, ili kuokoa maisha na mali za watu. Sababu nyingine ya ajali barabarani ni kutokana na ufinyu wa barabara nyingi ambazo hadhikizi ongezeko la magari kwa sasa. Hii ni changamoto kwa Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba; wanalitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la chanzo cha ajali barabarani pamoja na kuweka kikosi cha uokoaji, kwani Wananchi wengi wanaweza kuokolewa, ikiwa kama msaada utafika kwa wakati unaofaa.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Kikwete, Rais wa Tanzania, Mh.Bernard Membe....Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alisema; Serikali imeshitushwa na vifo vya Ndugu Wakapuchini na kwamba; Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Wamissionari katika harakati za Kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu Kiroho na Kimwili; hususani katika sekta ya Afya na Elimu.

Serikali imekwisha tuma salamu zake za rambi rambi kwa Wizara ya Mambo ya nchi za nje na Ushirikiano wa Kimataifa - Italy.....kutokana na vifo vya Wamissionari hawa ambao wote walikuwa wanatoka Italy.

No comments:

WATEMBELEAJI