Monday, November 21, 2011

TEDY NA PETER...WAZEE WA KAZI, NITAWAKUMBUKA DAIMA!

Huu msalaba upo Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida. Huu msalaba una historia sana....hasa kwangu mimi, maana jamaa alioujenga huu msalaba ni mtu ambaye nilikuwa nampenda sana tena sana na kutaka kufanana nae kwa yote. Hasa kwa mambo ya kazi, jamaa alikuwa na wito sana wa kufanya kazi....kazi zote alikuwa anafanya bila shida, na ni mtundu sana wa kugundua na kufumbua kazi mbalimbali. Jamaa anaitwa Tedy kutoka Canada, alikuja Tanzania kufanya kazi katika Misheni....alifanya kazi mbalimbali hasa za kuchimba visima katika CPPS - Water Project -Dodoma, sehemu ambayo nilifanyakazi pia mimi huko Dodoma. Tedy alikuwa ni msomi na kuwa na ujuzi mbalimbali kama vile wa kuendesha ndege ndogo ya watu 6, na ndege hiyo aliyokuwa akiendesha Tedy..... Baba yake mzazi alitoa zawadi kwa Misheni kwaajili ya kusafirishia wagonjwa na matumizi mbalimbali ya kazi za Jamii ya Tanzania. Lakini Tedy alikuwa akinifurahisha sana pamoja na usomi wake....lakini kufanya kazi za kuchafuka kazi ngumu humwambii kitu, yeye yupo tu. Kwakweli alinigusa sana wakati huo nikiwa mdogo nilitamani sana kufanya kazi na Tedy. Nilikuwa nikimwona akichapa kazi si mchezo, asubuhi mpaka jioni...tena kazi ngumu, nikasema napenda sana kuwa kama Tedy , ndoto yangu ilikuwa hiyo kufanana naye; lakini ni vigumu sana kufanana naye huyu jamaa... maana jamaa alikuwa na nguvu za ajabu sana, alikuwa na nguvu sana ya kunyanyua vitu vizito, kupiga zenge bila kuchoka mpaka jioni, ukimpeleka kwenye kuchimba mitaru yumo tu! kila kitu alifanya. Familia tajiri kama ya Tedy...ingelikuwa Familia ya Kitanzania, asingechafuka hata kidogo; maana familia yake huko Canada wana kila kitu...mpaka kufikia Baba yake kuzawadia ndege shirika la Wamissionari si mchezo. Lakini jamaa hakujidai hata kidogo....yeye alijidai na kazi, maneno ya Tedy mara nyingi yalikuwa ni; KAZI YAKO NDIO JINA LAKO. Na ndiye aliyeandika maneno haya kwenye Compresa (Trela) ya Lori la Uchimbaji (BIG BRO). Alikuwa akisema; lazima watu wakuite wewe ni mchimba visima; kwahiyo hilo ndio jina lako hasa...au wewe Daktari, wengi wanakufahamu kama Daktari hasa ukiwa hodari, wengine hawafahamu hata jina lako, kwahiyo kazi yako inakuwa ndo jina lako. Ndio maana namkumbuka kwa hili na nikatoa jina hili la Blog hii ya KAZI YAKO NI JINA LAKO. Jamaa pia alikuwa ni mtu wa watu, huko Dodoma, Singida na vijiji vyake vingi wanamjua Tedy kwa kazi nyingi alizozifanya, ukiwepo huo msalaba wa Manyoni, alijenga peke yake upo juu sana ya mlima wa Mwanzi - Manyoni, na mlima huo una jiwe lipo juu sana....huwezi amini aliwezaje kujenga peke yake? Kwanza hilo jiwe kulipanda ni shida sana....yaani huwezi kulipata kirahisi, lakini yeye alipandisha vyuma vizito pamoja na zenge. Watu wakorofi alikuwa akiwanyoosha kweli kweli, anakudunda haswa ukimkorofisha.....alikuwa anapenda sana usemi; nitakukunja, na kweli anakukunja haswa, ila alikuwa ni mtu mpole sana mpaka umkorofi, utasikia tu nitakukunja! Uwanja wa ndege wa Tabora, alitua na ndege yake kwenda kusavei maji....ili kuchimba visima, jamaa mmoja uwanjani hapo akawa anamletea za kuleta, mbona huvai nguo za kirubani mara hivi na vile....Tedy alimwambia mimi nimekuja kufanyakazi muhimu ya kutafuta maji kwa kusaidia watu wenye shida ya maji, kwahiyo naomba sana niende kufanya kazi iliyonileta ili nilete malori ya uchimbaji maji mapema iwezekanavyo kusaidia watu, mavazi ni nini mbona mimi najua kuendesha ndege?, jamaa akawa haelewi somo, mara Tedy akakasirika nitakukunja.....na kweli; alimshika kwa mkono mmoja na kumnyanyua juu, jamaa hakuongea kitu tena....alikuwa akiona ndege ya Tedy inatua anakimbia, na anabaki kusema lile zungu balaa. Kwakweli Tedy alinifunza mambo mengi sana ya maisha, kuishi maisha na watu bila kunyanyasa watu hata kama unauwezo, kufanyakazi bila kuchagua, ooh mimi nimesoma siwezi kuchafuka, mara hivi na vile....pia mtu mwingine ambaye ni kama Tedy hana tofauti ni Peter ambaye yeye anatoka Austria mpakani mwa Italy na Austria, pia yeye ni balaa kwa kazi na ujuzi mbalimbali hivyo hivyo kama mwenzake Tedy. Baada ya Tedy kurudi Canada alishika Water Project- Peter.....hawa jamaa walikuwa wanafanya kazi zaidi yetu sisi vibarua, na ukitukuta baada ya kazi utafikiri sio mabosi wetu, tulivyokuwa tukitaniana....lakini kwenye kazi ni kazi tu! kwenda mbele. Peter alinifundisha kuendesha Lori sikutegemea, alikuwa akiniambia ujuzi zaidi hauleti magonjwa, unasaidia sana, ni kweli kabisa kuwa na ujuzi mwingi ni raha sana pia ni msaada mkubwa sana katika maisha. Hawa jamaa wawili mimi kwangu ni walimu wakubwa sana katika kazi na katika maisha kwa ujumla....sita kuja niwasahau daima! Tedy sina mawasiliano naye sana....kutokana na majukumu aliyonayo huko Canada.....mara kwa mara anaenda Guatemara kusaidia kazi mbalimbali za jamii ya huko...hasa za uchimbaji visima, kujenga matenki ya maji n.k....kama alivyokuwa akifanya Tanzania, mara nyingi yupo bize sana, lakini Mwalimu Peter...mpaka sasa huwa namwita Mwalimu, yeye mara nyingi tunaongea kwenye simu na nipatapo tu! nafasi huwa naenda huko kwake Austria kumtembelea na kumsaidia kazi mbalimbali ili niendelee kuimba ujuzi mbalimbali....hata hivi kesho naenda kwake kwa wiki moja mpaka Jumatatu ndipo nitarudi.

Tedy...akipiga zege ya kujengea fensi ya Misheni ya Manyoni. Alikuwa pia anapenda msemo wa zege hailali....hivyo anapiga kazi mpaka usiku mpaka zege iishe. Sio tu zege....ulikuwa ni msemo wake wa kuendelea kufanya kazi.



Tedy.....kwenye (Lori) mtambo wa uchimbaji visima akiwajibika kutafuta maji enzi hizo huko Mbweni - Dar es salaam.





Peter.....kwenye utoaji wa pampu kwa mkono huko Kijijini Singida, mita za kutosha kweda chini...wakati huo kulikuwa hakuna wichi ya kutolea au kushusha pampu kama sasa. Jamaa ana nguvu na akili mpaka basi.







Na mimi nikijaribu kidogo kutafuta maji, mashine hii hii wametumia Tedy na Peter mpaka sasa ipo na inatunzwa sana.... hapa katika kuchimba kisima; mwaka jana huko porini kijijini ndani ya Itigi - Singida. Kisima cha Wachina kwaajili ya ujenzi wa Barabara ya Manyoni - Itigi - Tabora.









Tedy na mkewe Miriam (katikati) mwenye mtoto, na kwa pembeni ni mke wa Peter- Anna, mama wa ubatizo. Ni mtoto wao katika ubatizo uliyofanyika Dar es salaam enzi hizo...kwasasa mtoto huyu ni msichana wa miaka 18. Kama tunavyoona hapa Tedy alikuwa kapanda si mchezo......nguvu za kazi ndo usiseme kabisa....nimesikia bado anaendeleza libeneke.











No comments:

WATEMBELEAJI