Monday, November 21, 2011

WAUMINI WAMKATAA ASKOFU-ANGLIKANA......

........WAMZUIA KUINGIA KANISANI KUONGOZA IBADA.

Sakata la Waumini wa Kanisa la Anglikana Kilimatinde, Wilayani Manyoni, Mkoani Singida....kumkataa Askofu wa Dayosisi ya Rift Valley, John Lupaa...limechukua sura mpya baada ya kumzuia kuingia Kanisani ili kuongoza ibada.
Askofu Lupaa alifika katika majengo ya kanisa hilo akiwa na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari, lakini alishindwa kuingia na kuongoza ibada baada ya baadhi ya waumini kusimama milangoni ili kuzuia asiweze kuingia.

Askofu alisema; ''Jamani wale waumini ambao mpo tayari kuwa pamoja nami, njooni katika chumba cha darasa ili tuendelee na ibada, wale wasiotaka kuja basi waingie kanisani kuendelea na ibada kama kawaida. ''Askofu Lupaa aliwasihi waumini hao.
Kanisa hilo la Kilimatinde lipo jirani sana na shule ya Msingi ya Kilimatinde, hivyo aliwaomba wale wanao mkubali wamfuate darasani, shuleni hapo ili wakasali pamoja naye.

Baadhi ya waumini wanaomkubali walikwenda katika chumba cha darasa tayari kwa ibada ambayo iliongozwa na Askofu huyo, na wengine wasiomkubali waliingia kanisani na kuendelea na ibada yao. Waandishi ambao waliongozana na Askofu Lupaa, nao walikataliwa kuingia Kanisani hapo na kutakiwa kuondoka kabisa katika eneo hilo kwa tuhuma ya kununuliwa na Askofu huyo.

Waumini walisema; ''Tuna taarifa kuwa Askofu Lupaa amewanunua baadhi ya waumini na wandishi ili waje kumsafisha, mkakati huu tumeugundua, hatuwezi kuwaruhusu muingie kanisani, hatuna imani ndio maana mmekuja katika gari moja.''
Sakata la waamini na waandishi kutoruhusiwa kuingia kanisani ili kupata kiini cha mgogoro uliopo, lilidumu kwa dakika 15 lakini baada ya kujieleza vizuri, waliruhusiwa kuingia kanisani ili kushiriki ibada.
Waumini wa Dayosisi ya Rift Valley, hawamtaki kabisa Askofu huyo....ilisikika pia alishakataliwa kuingia kanisani kwaajili ya kuongoza ibada, sehemu mbalimbali za Dayosisi hiyo.

Askofu Lupaa; alitumia fursa hiyo kuwataka waumini wote wa Kanisa hilo, kutochukua sheria mkononi badala yake wajenge utamaduni wa kutumia demokrasia wanapodai haki zao.

Askofu Lupaa alisema; nashangaa sana kuona mwenye mali anazuiwa kuingia katika majengo yake, mimi ndiye mwenye mali kwa niaba ya Maaskofu wengine, nimezuiliwa kuingia kanisani nisali hadi nikalazimika kuingia darasani ili siku isinipite. Aliwataka waumini ambao wanamuunga mkono, kufanya maombi pamoja na kupuuza madai yanayotolewa dhidi yake na baadhi ya waumini wa kanisa hilo.

No comments:

WATEMBELEAJI