Tuesday, December 6, 2011

NIMEPOKEA SASAHIVI TAARIFA YA MSIBA WA BABU YANGU!

Nimepokea sasahivi simu kutoka nyumbani Kijijini....taarifa ya msiba wa Babu yangu Mpendwa Mzee Blezi Chibiriti, kuwa hatunaye tena...na taarifa zaidi za mazishi ni hapo kesho. Kwakweli nimehuzunika sana, maana ni Babu niliyekuwa nampenda sana..kutokana na kuishi naye kwa muda mrefu huko Kijijini, na alikuwa ananipenda sana tena sana...alisema mara kwa mara kati ya Wajukuu wake wote Mimi na Binamu yangu Dino, mtoto wa shangazi yangu, ambaye alikuwa mtoto wa Babu wa pili, ndio tulikuwa tunapendwa zaidi; alisema kuwa sio wengine siwapendi; lakini sisi ni zaidi. Hata mimi hamasa yangu kubwa kila nifikapo Tz iwe isiwe lazima ilikuwa nifike kwa Babu. Kwakweli amejariwa kuishi miaka mingi sana na mpaka mara ya mwisho kumwona mwezi wa nane mwaka huu, alikuwa bado mwenye nguvu sana tu...alikuwa akienda shambani bado. Alikuwa ni mwenye kupenda kazi sana tena sana mpaka mwisho wa mwisho na uzee wake alikuwa bado akishika jembe begani na kwenda kulima shambani....alipenda kusema utajili wangu mimi ni mashamba tu! Sisi tulisema mbona hayakupi faida yoyote, yeye alijibu; Yananipa faida kubwa sana ya kuuweka mwili imara na kutowaza mambo mengi bila ya sababu...kazi ilimfanya aishi vyema na mwili kuutunza, ni faida kubwa sana hii..alisema Babu. Pia yeye alipenda sana kunywa chai daima...ukienda bila zawadi ya sukari na majani ya chai kwake hujamzawadia kitu. Ni Babu ambaye nitamkumbuka sana katika maisha yangu yote...hasa kwa kunifundisha mambo mengi sana ya maisha haya ya kuishi na watu, kupenda kusali n.k. Amepata bahati sana ya kuishi miaka mingi sana..wakati wazee wa lika lake wote Kijijini kwetu walishatangulia mbele ya haki, alibaki yeye. Nimesikitika sana, ni kawaida ukipotelewa na mtu umpendaye....lakini pia ninafuraha kwaajili yake Babu; maana yeye alisema mara kwa mara; ukiishi miaka mingi huna budi kumshukuru Mungu na kumwomba akuite kwa kifo cha raha ili upumzike kwake, hivyo siku nikiondoka usinikumbuke kwa uzuni sana bali kwa furaha, ukihuzunika sana utakuwa kama unamkufuru Mungu kwa mambo mengi, kwanza kunifahamu...wengine hawana bahati ya kuwafahamu Babu/Bibi zao...hivyo ni jambo la kushukuru. Pia kila mara tulitaniana hivi; Kila nikienda likizo nikimkuta aliniambia; tripu ijayo nitakufanyia utani wa kutonikuta tena, bali utaona kichukuu changu (Kaburi). Lakini karibu miaka 10 sasa namkuta tu. Na mimi nilimwambia Babu mimi ndio ninakutania sana, nakukuta kila nikija wewe huondoki sasahivi, wewe ni wahapa hapa bado...tulicheka sana na kufurahi. Lakini sikuwahi kusikia alalamike kuwa ana shida ya kuumwa wale nini, ni bahati sana kwa nyakati hizi kuwa na afya jema namna hii, hata nilipoenda mara ya mwisho mwezi 8 mwaka huu alikuwa fiti kabisa. Ila sasa kweli kanitania kwa utani huu wa Kifo chake....haya bwana Babu umeshinda wewe tripu hii. Na Mwenyezi Mungu awe nawe...akutangule katika safari yako ya kwenda huko Mbinguni kwake, na akulaze mahali pema peponi....amina! Na usitusahau katika maombezi yako.....Safiri salama Babu Chibiriti.
Picha ya Babu Blezi Chibiriti, akiwa na mwanae wa mwisho mpendwa wake Fabiani Chibiriti...kwenye Fani ya Fabiani mbele ya Lori la Fabi, enzi za nyuma kidogo...wakati Babu alipofika Jijini Dar es salaam..... kuosha macho kidogo Town. Alikuwa akituchekesha sana alisema; naomba mnipeleke Dar es salaam nikatembee kidogo na kuosha macho, akifika Dar es salaam baada ya siku mbili naomba nirudi Kijijini....mbona ndo umefika tu Babu? ukae kae kidogo, jibu ni hakuna hiyo....alikuwa anazila mpaka kula nirudisheni nyumbani huku sikuwezi kabisaa!!!!

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

mimi pamoja na familia yangu tunapenda kuwapeni pole wafiwa wote kwa msiba wa babu yetu Blezi. Kaka Baraka pole sana. Pia katika malezo yako nilikuwa nasoma huku nalia na kucheka kwa jinsi ulivyokuwa na utani na babu...Na najua sasa unamkumbuka sana lakini kama ulivyosema sasa yupo anapumzika na wala hatakusahau katika maombezi yake na Mama Bikira Maria atamsaidia pia. Nimefurahi sana kusikia babu alikuwa akipenda chai...Ustarehe kwa amani babu yetu Blezi Chibiriti.

Baraka Chibiriti said...

Asante sana Dada Yasinta, nashukuru mno kwa kunifariji...maana usiku sikulala kabisa, wakati mwingie machozi yalikuwa yakinitoka, wakati mwingine nacheka tu! Ndo hivyo Mungu amsamehe kwa mapungufu yake na ampumzishe kwa amani....Amina!
Asante sana Dada Yasinta.

WATEMBELEAJI