JUBILEE YA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA, KIWE NI KIPINDI CHA SHUKRANI, TOBA, MSAMAHA NA UPATANISHO!
Kuna haja kwa Watanzania wote....wakati huu tunapojiandaa kwaajili ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka hamsini tangu tulipojipatia uhuru wa bendera; kufunga na kusali....ili kuomba toba na huruma ya Mungu kwa mapungufu yaliyojitokeza katika maisha ya kila mtu mmoja mmoja na kama Jamii ya Watanzania.
Ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka alizotukirimia Watanzania hata bila mastahili yetu. Kwa namna ya pekee Watanzania tunapaswa kujikita zaidi katika mchakato mzima utakaodumisha amani ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Umoja , upendo na mshikamano wa Kitaifa....tunu ambazo Waasisi wa Tanzania na kwa namna ya pekee, Mwalimu Julius kambarage Nyerere alituachia Watanzania kama sehemu ya urithi wetu endelevu na nguzo msingi kwa nchi ya Tanzania.
Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa kisiwa cha amani na bandari salama kwa watu wanaotafuta makazi kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Afrika, na kwa hakika Tanzania imeonyesha mfano wa kuigwa kwa njia ya ukarimu huu. Ni dhamana ya sisi Watanzania kuhakikisha kwamba; Tanzania inaendelea kuwa ni kisiwa cha amani, upendo na mshikamano wa Kitaifa; dhidi ya ubinafsi, udini, ukabila na umajigambo....mambo ambayo yanatishia misingi ya Taifa letu la Tanzania.
Watanzania pia tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mchango wa sala katika kuwendeleza mwanadamu kiroho na kimwili. Hii ndiyo dhamana ya kina inayogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili; kwa kutambua na kuthamini utu na heshima ya kila mwanadamu...aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu.
Zawadi ya maisha, utu na heshima ya mwanadamu...vikiheshimiwa na kuthaminiwa, Tanzania inaweza kuendelea kuwa ni kisiwa cha amani na mshikamano hata baada ya Jubilee ya miaka hamsini ya uhuru wa Tanzania. Amani iliyoko Tanzania inatuwajibisha Watanzania wote kulinda na kuidumisha kwaajili ya ustawi na maendeleo ya Tanzania, afrika na ulimwengu kwa ujumla.
- MWENYEZI MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE WOTE.
No comments:
Post a Comment