BENKI YA MKOMBOZI INAPANIA KULETA UKOMBOZI KWA WATANZANIA WA KIPATO CHA CHINI.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa mstari wa mbele katika harakati za kulitegemeza Kanisa kwa njia ya miradi mbali mbali inayobuniwa na kundeshwa na Baraza hilo.
Kanisa Katoliki limekuwa mdau mkubwa katika masuala ya elimu kwa kuanzisha mfumo wa elimu kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu. Mwelekeo huu unajionyesha pia katika sekta ya afya na maendeleo endelevu. Lengo hasa anasema Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es salaam, ni uinjilishaji wa kina unaopania kumhudumia Mtanzania katika mahitaji yake ya kiroho na kimwili.
Hivi karibuni Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limezindua Benki ya Mkombozi, itakayoendeshwa kibiashara kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kiuchumi bila kujali imani, itikadi na mahali wanapotoka. Tanzania katika miaka ya hivi karibuni imeshuhudia kupanuka pengo kati ya wananchi wa kipato cha juu na wale wa kipato cha chini. Benki ya Mkombozi inalenga hasa kuwawezesha waanchi wa kipato cha chini, kuweza kujimudu katika maisha yao.
Mikakati ya kulitegemeza Kanisa Katoliki Tanzania ni kati ya mambo yanayoendelea kushika kasi, hasa baada ya Kanisa kwa miaka mingi kutegemea ufadhili kutoka Vatican na mashirika mengine ya misaada. Sasa linaona kwamba umefika wakati wa kutumia rasilimali iliyopo kwa ajili ya maendeleo ya watu nchini Tanzania. Kardinali Polycarp Pengo anawaalika Watanzania kufungua akiba zao katika Benki ya Mkombozi, ili waonje mabadiliko yanayolenga kuwakomboa kiuchumi.
Benki ya Mkombozi ambayo ina makao yake makuu Jijini Dar es salaam, imekuwa ikifanya kazi kwa majaribio tangu mwezi Agosti, 2009. Kwa kushirikiana na Benki nyingine Tanzania, hali ambayo inawawezesha wateja wa Benki ya Mkombozi kupata huduma kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania. Ni ufafanuzi uliotolewa na Mama Edwina Lupembe, mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Mkombozi.
Benki imeanza kwa mtaji wa Billioni 6.5 hadi sasa mtaji huu umekuwa na kuongezeka hadi kufikia Billioni 9. Hadi sasa Benki ya Mkombozi imekwisha toa mkopo wa millioni 637 na imewekeza kwenye Benki nyingine kiasi cha Billioni 6.3 tangu ilipoanza kufanya kazi yake. Benki ya Mkombozi inatoa mikopo ya elimu na kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, lengo kubwa zaidi ni kupambana na umaskini wa kipato na ujinga na maradhi ili kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli.
Mama Lupembe anasema; kwa namna ya pekee Benki ya Mkombozi inapania kuwawezesha wakulima wadogo wadogo ambao mara nyingi wamekuwa wakisahaurika na Taasisi za Fedha, ili kwenda sambamba na sera ya Serikali inayotoa kipaumbele kwa kilimo, yaani KILIMO KWANZA. Mkulima anahitaji kiasi cha shilingi elfu kumi na tatu za kitanzania kufungua akiba yake katika Benki hii ya Mkombozi.
Benki ya Mkombozi ilizinduliwa rasmi na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi aliyelipongeza sana Kanisa Katoliki kwa kutumia rasilimali ya Watanzania kabla ya kukimbilia msaada na mahitaji kutoka nje ya nchi yetu. Hii ni michango ya waamini kutoka katika Jumuia ndogo ndogo za kikristo hadi kufikia hatua hii nzuri.
1 comment:
ASANTE SANA BARAKA MWENYE BARAKA.
HII BENKI IPO HAPA JIRANI NA OFISINI KWETU.BENKI IPO MTAA WA MANSFIELD ZAMANI CATHEDRAL BOOK SHOP.
R.Njau
Dar es salaam
Post a Comment