.......KATI YA BWANA NA BIBI; UNAOFUMBATWA KATIKA HESHIMA, UAMINIFU, MAJITOLEO, USHIRIKIANO, UVUMILIVU NA UKOMAVU.
katika makala hii napembua kwa dhati misingi ya maisha ya ndoa, katika azma ya kujenga kwa upendo mapendano ya wana ndoa na majitoleo ya mtu. Ndoa si lele mama...yahitaji majiundo makini, uvumilivu na moyo mkuu. Msingi mkuu wa maisha ya ndoa ni upendo wa dhati wa wanandoa wenyewe, wapendane kama walivyo. Ni jukumu la kila mwanandoa kuutunza upendo huo, kuupalilia, ili ukue vema na kudumu na uzae matunda, ili upendo wa wanandoa upate kudumu kwa ukweli, unahitaji mambo yafuatayo;
1). HESHIMA KWA KILA MMOJA (HAKUNA ALIYE ZAIDI YA MWENZAKE).
Kila mwanandoa atambue na kuthamini uwepo wa mwenzake katika familia na kujali matatizo na furaha za mwenzake. Usimfanye mwenzio kama chombo tu cha matumizi ndani ya nyumba, mpe hadhi na heshima yake.
2). UAMINIFU KWA KILA MMOJA.
Uaminifu na kuaminiana vina maana na uzito wa pekee kabisa katika maisha ya ndoa. Kila mwanandoa ajitahidi kuwa mwaminifu kwa mwenzi wake. Kila mmoja awe mwaminifu katika mahusiano ya ndani, pia awe mwaminifu katika kutimiza mipango ya uchumi na maendeleo ya familia. UAMINIFU NI SABUNI YA MAHUSIANO YASIYO NA WASIWASI.
3). KUSAIDIANA NA KUSHAURIANA (KUBALI USHAURI WA MWENZIO).
Kila mmoja ni msaada kwa mwenzake, si vema kuona kwamba mwenzako ''hana maana kwako'' Mungu alikupa huyo kama msaidizi mwenye kufanana nawe. Umshauri nawe pia ukubali akushauri. Hata kama unamwona duni na mnyonge vipi, si ulimpenda mwenyewe? Iweje leo umwone kuwa hafai tena na hutaki ushauri wake? Hutaki kazi zake? Kumbuka;
HATA NG'OMBE MWEUSI HUTOA MAZIWA MEUPE.
4). KUSHIRIKIANA MIPANGO MBALIMBALI (USIRI NI SUMU KATIKA NDOA).
Wanandoa wapende daima kushirikishana mipango mbalimbali ya uchumi na maendeleo katika familia. Katika hali ya kawaida, si vema sana kwa wanandoa kufichana mipango yao...jambo laweza kuwa zuri sana lakini kama halikushirikishwa kwa mwenzi, basi linakuwa na harufu ya ubovu na hatimaye ni chanzo cha sokomoko na malumbano katika ndoa yenu.
5). KUVUMILIANA NA KUCHUKULIANA MLIVYO.
Wanandoa wanapaswa kusaidiana kukua, sio kila jambo litakubalika tu na mwenzi. Kuna mengine wanandoa wanaweza kurekebishana/kusahihishana kwa upendo. Kuna mengine watashindwa kabisa kurekebishana, hayo yanayoshindikana kabisa...basi uvumilivu wa kweli uchukue nafasi yake.
NDOA ZINAZODUMU NI ZA WATU WAVUMILIVU TU!
6). KUJENGANA NA KUSAHIHISHANA KWA UPENDO.
Kama nilivyokwisha kusema hapo awali, yawezekana katika maisha ya kila siku wanandoa wakakoseana na wakakoseana katika mamo mbalimbali, iepukwe kila namna ya kushabikia, kubeza au kuzomea kosa la mwenzi wako. Badala yake wanandoa wajenge hulka ya kuoneana huruma, kujengana katika utu wema na kusahihishana kwa upendo.
KUMBUKA; AIBU YA MWENZIO NI YAKO PIA.
7). KULINDA KUTA ZA NYUMBA.
Hili ni jambo la maana sana katika maisha ya ndoa, maisha ya ndoa yanahitaji ukomavu wa hali ya juu sana katika kuijenga nyumba na kuilinda. Kila mmoja akijitahidi sana kulinda kuta za nyumba yao wenyewe, hapo watailinda heshima ya ndoa yao. Katika hili naongelea haswa juu ya UTUNZAJI WA SIRI NDANI YA NDOA. Ni aibu kubwa sana kwa wewe mama au baba kuanika siri za Mmeo/Mkeo hadharani, kufanya hivyo ni kumfungulia shetani mlango, pia ni kuhatarisha ndoa yenu wenyewe na tena ni kujidhalilisha ninyi wenyewe. Mambo ya ndani yabaki ndani. Hata kama yatakuwa ni lazima sana yatoke...yatatoka kwa busara kuu sana.
WANANDOA WALIO WAKOMAVU, DAIMA WANAHESHIMU SIRI ZAO ZA NDANI YA NYUMBA YAO.
- Kweli kabisa mara nyingi husikia maneno ya ajabu ya wanandoa, mpaka unabaki unashangaa kwanini iwe hivyo? Tena unakuta watu wengine ni wastarabu kabisa....lakini wanakosa kabisa ustarabu wao kwa swala kama hili.
Ndugu zangu wanandoa, tuzitunze ndoa zetu ili tupate kuzijenga vema familia zetu. Familia yenye afya njema hujengwa katika msingi wa ndoa bora, ndoa imara. Katika famila hiyo iliyo bora, wanafamilia husali pamoja, hufurahi pamoja na huweka nia moja kwa maslahi ya familia. Maisha ya ndoa ni wito, wenye kuuishi vema wito huo; wanamtukuza Mungu, na wao wenyewe wanatakatifuzwa.
No comments:
Post a Comment