Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es salaam, mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema kuna kila dalili za kukwama kwa mkakati wa kilimo kwanza, kutokana na kushindwa kuelekeza nguvu za kutoa elimu kwa wakulima ili waendeleze sekta hiyo vizuri.
Kardinali Pengo alitoa kauli hiyo juzi katika hafla ya kuzindua jengo jipya la maabara katika chuo cha Teknolojia ya uhandisi cha Mtakatifu Joseph kilichopo Mbezi Luguruni Jijini Dar es salaam.
Jengo hilo limepewa jina la: HIS EMINENCE POLYCARP PENGO BLOCK. Kauli ya Kardinali Pengo inakuja wakati Serikali imekuwa ikielekeza nguvu nyingi katika kutekeleza mpango huo mkubwa, ikiwa ni pamoja na kusambaza matrekta Mikoani. Akionyesha mtizamo huo tofauti Pengo alisema, ''kaulimbiu inayotumiwa na viongozi wa nchi (kilimo kwanza) haiwezi kubadili au kuleta maendeleo yoyote katika kilimo cha msingi, hapa ni kumwezeshamkulima kwanza ili apate elimu ya kuendeleza kilimo, ni vigumu kufikia azma ya kilimo kwanza bila kuwawezesha wakulima kwa kuwa na mabadiliko ya kimaendeleo katika nyanja ya kilimo inapatikana kwa mkulima wenye elimu.
Pengo ambaye ni nadra kuzungumzia utendaji wa Serikali, alisema kilimo kimekuwa kikizungumzwa kama wimbo tu, bila kuweka nguvu na mkazo katika utekelezaji wenye kuwawezesha wakulima ambao ndiyo wahusika wakuu.
Alisema jambo hili linachangia ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hasa maeneo ya vijijini. Kwakua kilimo kimekuwa kikizungumzwa tu kama wimbo, vijana wengi wamekuwa wakiondoka vijijini na kukimbilia kwenye miji mikubwa kama Dar es salaam, wakifikiri watapata maisha bora, kumbe wanajikuta wakikutana na ugumu wa maisha na kupoteza mwelekeo wao kabisa.
Kiongozi huyo wa kiroho wa Kanisa Katoliki, alisisitiza kuwa Serikali ina wajibu kuhakikisha elimu ya kilimo inaifikia jamii na kumwezesha mkulima kwanza.
No comments:
Post a Comment