Leo nimekumbuka sana kazi yangu ya zamani, ya uchimbaji visima vya maji masafi ya kunywa huko vijijini Tanzania, ambapo kuna ukame sijapata kuona na shida ya maji sana mpaka unatamani kulia wakati mwingine kwa kuwaonea huruma wananchi katika shida hii ya maji. Kazi hii niliifanya kabla sijaja huku Ulaya, kazi hii niliifanya kwa moyo wote na kwa nguvu zangu zote, maana ilikuwa ni ya mtulinga sana, lakini niliipenda sana na mpaka sasa bado ninaipenda sana. Nilikuwa si mimi peke yangu na wenzangu wanne tukiongozwa na Peter Schwingshackl ambae alikuwa Boss wetu wa kitengo hiki cha uchimbaji visima (CPPS WATER PROJECT). Kwakweli Peter alikuwa Boss wetu jina tu, yaani alifanya kazi zaidi ya wafanyakazi wake, tulihangaika nae daima huko vijijini kwa kazi hizi ngumu na matatizo mbalimbali ya vijijini, kama mnavyojua vijijini kulivyo, yeye alikuwa mstali wambele kabisa! Nimejifunza mengi sana kwake katika kazi na hata katika maisha kwa ujumla, maana alikuwa na uwezo lakini alijitolea kwaajili ya kusaidia watu. Mpaka tulikuwa tukimwuliza wakati mwingine, kwanini unahangaika wakati huna shida kabisa, yeye alijibu daima; maisha ni nini? Maisha ni watu....usipo jitolea kusaidia watu si maisha tena ni ubinafsi tu! Tulikuwa tukimwita kwa jina la; Mwalimu. na kweli alikuwa mwalimu hasa, kwasasa alirudi kwao na familia yake, yeye na mkewe na watoto wake. Kwasasa wanaishi huko Welsberg - Monguelfo, mpakani mwa Italy na Austria.
Sasa leo nimepata simu kutoka kwa wafanyakazi niliokuwa nikifanya nao kazi, mpaka nimetokwa na machozi sikuamini kama ningepata simu kutoka kwao, na wakiniomba siku nikiamua nirudi tena pamoja nao. Nimefurahi sana na kukumbuka sana kazi hii ya uchimbaji visima. Wamenipigia simu wakiwa Mkoani Tabora, wakijimba maeneo ya Kiparapara. Kila Lakheri kwa kuhudumisha huduma hii ya maji vijijini, ili Tanzania tuweze kuondokana na hali mbaya ya ukame wa maji ya kunywa.
-Nami nawaahidi kwa moyo wote ipo siku nitalejea tena katika kazi hiyo na kuwa pamoja kwa lengo moja la kusaidia vijiji vyenye uhaba wa maji.
No comments:
Post a Comment