Friday, March 18, 2011

UTU NA HESHIMA YA MWANADAMU!

Utu na Heshima ya mwanadamu ni muhimu sana kuliko mambo yote; Tukazie umuhimu huu wa kulinda na kutunza Utu na Heshima ya mwanadamu. Lengo ni kuhakikisha kuwa Jamii inafanikiwa kupata mafao ya wengi, kwa kutoa vipaumbele vitakavyo waongoza katika maisha yote.
Utu wa mwanadamu unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kabisa katika mikakati ya maendeleo endelevu katika Dunia hii, kwani binadamu ameubwa kwa sura na mfano wa Mungu, na kila mwanadamu ana faida sana hapa Duniani, hakuna asiye faa hata mmoja!, tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika.
Hii ni changamoto ya kulinda na kuheshimu zawadi hii ya maisha, changamoto inayokwenda sambamba na mapambano dhidi ya baa la umaskini, huduma bora za afya na fursa makini zitakazowawezesha watoto kukuza karama na vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, katika mchakato wa makuzi ya utu uzima.
Kulinda zawadi hii ya maisha ni jukumu linalokwenda sanjari na uimarishaji wa tunu msingi za maisha bora ya kifamilia kwa kutambua kwamba; Familia ni msingi wa Jumuiya ya Jamii bora zaidi. Itolewe changamoto zaidi kwa Serikali kuhakikisha kamba watu wanapata huduma bora za afya, bila kusahau kutoa msaada na huduma kwa walemavu ambao ni sehemu ya Jamii yetu, ili walau kila mtu aweze kuishi maisha yenye hadhi kama binadamu.
Jamii yetu inahitaji sana uchumi imara, ilikuwawezesha wananchi kupata mahitaji ya msingi kwa njia halali, vinginevyo amani na utulivu vinaweza kutoweka, hali ambayo inakwamisha jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu katika mafao ya wengi, ni jambo la msingi sana katika mikakati na sera za kisiasa katika mchakato wa kujenga Jamii inayosimikwa katika misingi ya Haki, Usawa na Utawala bora na unaozingatia sheria na haki msingi za binadamu. Upepo wa mabadiliko unaoendelea kujitokeza sehemu mbalimbali za Dunia hii ni changamoto ya kudumisha misingi ya Uwazi, Utu na Maadili mema katika masuala ya kiuchumi na kisiasa. Tulinde vizuri sana na kudumisha misingi ya Haki na Amani daima!

- B.F.Chibiriti.

No comments:

WATEMBELEAJI