Monday, September 26, 2011

DHAMANA NA UMUHIMU WA KAZI KATIKA MAISHA!

Kazi ni sehemu ya asili ya mwanadamu iliyofuata baada ya anguko lake, hivyo kazi sio adhabu wala laana. Katika mafundisho mbalimbali kwenye vitabu vilivyo vingi yanasisitiza kwamba lazima kuithamini na kuiheshimu kazi.
Mimi binafsi nalaani sana kwa mtumishi asiye na faida, anayeficha vipaji vyake....na kumsifia mtumishi mwaminifu na mwenye akili ambaye Bwana wake atamkuta akiwa anafanya kazi yake kwa bidii kutimiza majukumu aliyokabidhiwa. Mimi naweka bayana kuwa wito wangu ni kufanya kazi kwa bidii zote kadiri ya wito wa Mwenyezi Mungu. Kumbe tunapozifanya kazi zetu lazima kutambua kuwa kazi ni wito na neema toka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo lazima kumtanguliza Mungu, kwasababu wafanyao kazi bila Mungu wanajisumbua bure tu!
Ni katika ukweli huu, Yesu anamfundisha mwanadamu kwamba asiwe mtumwa wa kazi. Lililo muhimu zaidi ya yote ni kushughulikia na kujali roho yake. Yesu anakazia kuwa maana na lengo la maisha sio kuupata ulimwengu wote bila Mungu. Si sahihi kushindwa kutimiza wajibu wako kama mkristo eti kwasababu una kazi nyingi, si sahihi kushindwa kwenda kanisani siku za Jumapili na sikukuu zilizoamriwa eti kwasababu una kazi au unafanya biashara. Pia Yesu anafundisha kwamba kwakweli hazina ya duniani inatumika, wakati ile ya mbinguni haiharibiki kamwe. Ni katika hazina ya mbinguni ndipo lazima watu waweke mioyo yao. Hivyo kazi lazima isiwe chanzo cha shauku na kututia wasiwasi katika maisha, kwani zawadi na neema toka kwa Mungu isipotumika kadiri ya mapenzi yake inaweza pia kuwa kikwazo katika kumtumikia Mungu. Watu wanapokuwa na wasiwasi, mashaka na kutotulia kwasababu ya mambo mengi hapo wanaingia katika hatari ya kudharau na kuweka pembeni vitu ambavyo wanavihitaji kweli kwaajili ya ufalme wa Mungu na haki yake.

Kazi kama neema na zawadi inawasaidia watu kuwa huru kutoka minyororo ya mateso ya hapa duniani pale mwanadamu anapojitosheleza katika mahitaji yake ya kila siku. Kazi ya mwanadamu inayolenga kuzidisha au kuongeza nguvu na kugeuza ulimwengu ni lazima minyororo na kuachia uhuru mtimilifu ambao unapata asili na mfano wake katika Kristo mwenyewe. Ulimwengu wote umeumbwa katika yeye na kwa njia yake na kukombolewa naye kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Huu sio mkusanyiko wa vitu uliotokea kwa bahati nasibu, bali ni ulimwengu uliopangwa ukapangika ili kuonesha kazi ya uumbaji uliofanywa na Mwenyezi Mungu. Ni wajibu wa mwanadamu kugundua utaratibu uliomo katika ulimwengu na kufuata utaratibu huo na kuuwezesha ufike utimilifu katika Yesu Kristo, kwani ni katika yeye ulimwengu unaonekana kuumbwa kwaajili ya mwanadamu. Kazi inaeleza upande wa uwepo wa mwanadamu ulio muhimu kabisa wa ushiriki na sio tu katika tendo la uumbaji, bali pia katika tendo la ukombozi. Wale wanaopokea ugumu wa kazi kwa kuunganisha na Yesu wanashiriki kwa namna fulani na mwana wa Mungu katika kazi yake ya ukombozi na kuonesha kwamba ni wanafunzi wa Yesu, ndio wanaochukua msalaba wake.

- Kazi ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu, lakini pia Mwenyezi Mungu ni muhimu sana tena sana katika maisha ya mwanadamu.

1 comment:

ray njau said...

Methali 31:1-31

1 Maneno ya Lemueli mfalme, ujumbe mzito ambao mama yake alimwambia ili kumrekebisha:

2 Niseme nini, ewe mwanangu, niseme nini, ewe mwana wa tumbo langu, niseme nini, ewe mwana wa nadhiri zangu?

3 Usiwape wanawake nguvu zako za uhai, wala njia zako kwa kitu ambacho hufanya wafalme wafutiliwe mbali.

4 Haifai wafalme, ewe Lemueli, haifai wafalme kunywa divai wala maofisa wakuu kuuliza: “Kileo kiko wapi?” 5 ili mtu asinywe na kusahau jambo lililoagizwa na kupotosha haki ya yeyote wa wana wa mateso. 6 Mpeni kileo mtu yeyote anayekaribia kuangamia na kuwapa divai watu wenye uchungu katika nafsi. 7 Acheni mtu anywe na kuusahau umaskini wake, na mtu asiikumbuke taabu yake tena.

8 Fungua kinywa chako kwa ajili ya mtu asiyeweza kusema, ili kutetea watu wote wanaopitilia mbali. 9 Fungua kinywa chako, hukumu kwa uadilifu na kutetea mtu mwenye kuteseka na maskini.

10 Mke mwenye uwezo, ni nani anayeweza kumpata? Thamani yake inapita sana ile ya marijani.

11 Moyo wa mume wake umemtegemea, wala hakuna faida inayokosekana.

12 Amemthawabisha mume wake kwa mema, wala si kwa mabaya, siku zote za maisha yake.

13 Ametafuta sufu na kitani, naye hufanya kazi yoyote inayopendeza mikono yake.

14 Amekuwa kama meli za mfanyabiashara. Huleta chakula chake kutoka mbali.

15 Tena huamka kabla usiku haujaisha, na kuwapa watu wa nyumbani mwake chakula na kuwapa vijana wake wa kike fungu lao lililoamriwa.

16 Amefikiria shamba, akalinunua; amepanda shamba la mizabibu kutokana na matunda ya mikono yake.

17 Amejifunga nguvu viunoni, naye ameitia nguvu mikono yake.

18 Ametambua kwamba biashara yake ni nzuri; taa yake haizimiki usiku.

19 Amenyoosha mikono yake kushika kijiti cha kusokotea uzi, nayo mikono yake mwenyewe imeshika gurudumu la kusokota nyuzi.

20 Amewanyooshea mkono wenye kuteseka, na mikono yake amemkunjulia maskini.

21 Hana wasiwasi juu ya watu wa nyumbani mwake kwa sababu ya theluji, kwa maana watu wote wa nyumbani mwake wamevaa mavazi mawili.

22 Amejitengenezea matandiko yenye mapambo. Mavazi yake ni ya kitani na sufu iliyotiwa rangi ya zambarau.

23 Mume wake ni mtu anayejulikana malangoni, anapoketi pamoja na wanaume wazee wa nchi.

24 Hata ametengeneza mavazi ya ndani na kuyauza, nao wafanya-biashara amewapa mishipi.

25 Nguvu na fahari ndiyo mavazi yake, naye anaucheka wakati ujao.

26 Hufungua kinywa chake kwa hekima, na sheria ya fadhili zenye upendo ziko katika ulimi wake.

27 Anaangalia shughuli za nyumba yake, wala hali mkate wa uvivu.

28 Wanawe wamesimama na kumtangaza kuwa mwenye furaha, mume wake husimama, naye humsifu.

29 Kuna binti wengi ambao wameonyesha uwezo, lakini wewe—wewe umewapita hao wote.

30 Uvutio unaweza kudanganya, nayo sura yenye kupendeza inaweza kuwa ubatili; lakini mwanamke anayemwogopa Yehova ndiye anayejiletea sifa.

31 Mpeni baadhi ya matunda ya mikono yake, nazo kazi zake na zimsifu malangoni.

WATEMBELEAJI